Messi kizimbani kwa kukwepa kulipa kodi
30 Mei 2016Baada ya kuisaidia Barcelona kushinda mataji mawili msimu uliokamilika, La liga na Kombe la Mfalme, mshindi huyo mara tano wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka na babake Jorge Horacio Messi watafikishwa mahakamani kuhusiana na kesi hiyo ambayo imemwandama tangu Juni 2013.
Kesi hiyo itaendeshwa hadi Juni 2 – siku ambayo Messi anatarajiwa kutoa ushahidi pamoja na babake. Vikao vya mahakama vinakuja siku chache tu kabla ya kujiunga na wachezaji wenzake wa Argentina kushiriki katika kinyang'anyiro cha Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini, maarufu kama Copa Amerika litakaloandaliwa Marekani.
Pulido aokolewa na polisi Mexico
Polisi ya Mexico imemwokoa mchezaji wa kandanda aliyetekwa nyara Alan Pulido, ambaye ameonyeshwa leo katika kikao kifupi cha wanahabari akitangaza kuwa yuko katika hali nzuri.
Polisi na maafisa wengine walisema Pulido, mshambuliaji mwenye umri wa miaka 25 anayechezea klabu ya Ugiriki ya Olympiakos, aliokolewa katika operesheni ya usalama iliyokamilika usiku wa manane katika mji wa mpakani wa kaskazini mashariki wa Tamaulipas. Pulido alichukuliwa na watu waliokuwa na silaha Jumamosi usiku wakati akirejea nyumbani kutoka kwenye tafrija.
Pulido, aliyekuwa katika kikosi cha Mexico kilichocheza Kombe la Dunia mwaka wa 2014 nchini Brazil, alitekwa nyara nje ya mji aliozaliwa wa Ciudad Victoria. Maelfu ya watu hutekwa nyara nchini Mexico kila mwaka, mara nyingi na magenge yanayohusika na ulanguzi wa dawa za kulevya
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef