Messi na babake watakiwa kufika mahakamani
21 Juni 2013Messi ametakiwa kufika mahakamani Septemba 17. Mahakama moja ya Uhispania katika mji wa Gava karibu na Barcelona jana ilikubali kesi hiyo iliyowasilishwa na mwendesha mashitaka wa umma Raquel Amada wiki iliyopita. Jaji alimtaja Lionel Messi kama mshukiwa katika uchunguzi wa kukwepa kulipa kodi na akamtaka mshambuliaji huyo wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina kufika mahakamani Septemba 17.
Uchunguzi wa kukwepa kulipa kodi
Kikao hicho cha kuskizwa kesi yake mwezi Septemba kitakuwa sehemu ya uchunguzi wa mwanzo kuhusiana na kesi hiyo, ili kubainisha kama kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka rasmi Messi au babake Jorge Messi kwa kosa la kukwepa kulipa kodi.
Madai dhidi ya Messi yanahusu mapato ya kodi ya mwaka wa 2007, 2008 na 2009. mwendesha mashitaka Amada alisema mnamo Juni 12 kuwa Messi alikuwa na deni la kodi la kiasi cha euro milioni nne kutokana na malipo aliyopata katika mauzo ya haki za picha yake. Jorge Horacio Messi anahudumu kama mmoja wa mawakala wa mwanawe tangu alipojiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 16 mnamo mwaka wa 2004.
Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Argentina ameimarika na kuwa jina maarufu kote ulimwenguni katika kandanda, mshindi wa mataji manne mfululizo ya Mchezaji bora wa mwaka wa FIFA na pia mshambuliaji bora zaidi katika historia ya klabu ya Barca.
Pia alikuwa mfungaji wa magoli mengi zaidi katika msimu uliokamilika wa ligi kuu ya soka Uhispania La Liga, kwa kufunga zaidi y agoli moja katika kila mechi na kuisaidia Barcelona kurejesha kabatini taji ambalo walipokonywa awali na Real Madrid mwaka wa 2012.
Mwandishi: Bruce Amani/ (AFP, AP)
Mhariri: Josephat Charo