Messi, Ronaldo na Ribery nani bora?
16 Desemba 2013Mshambuliaji wa Barcelona Messi ameshinda tuzo hiyo mara nne lakini lakini anaonekana kulikosa mwaka huu, baada ya msimu wake kuathirika kutokana na jeraha. Mchezaji wa Ufaransa Franck Ribery alikuwa sehemu ya timu ya Bayern Munich iliyotwaa mataji matatu mfululizo ya Champions League, Bundesliga na Kombe la Shirikisho la Ujerumani pamoja na Kombe la European Super Cup.
Mshambuliaji nyota wa Ureno anayechezea Real Madrid Christiano Ronaldo maarufu kama CR7 alishinda Ballon d'Or mwaka wa 2008 na amepigiwa upatu kulishinda tena mara hii. Mshindi atatajwa mjini Zurich Januari 13.
Jupp Heynckes aliyekuwa kocha wa Bayern Munich atawania taji hilo kwa upande wa kocha bora wa mwaka kwa upande wa wanaume, pamoja na kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson na Jurgen Klopp wa Borussia Dortmund.
Kwa wanawake, Ralf Kellermann (VfL Wolfsburg), Silvia Neid (timu ya taifa ya Ujerumani) na Pia Sundhage (timu ya taifa ya Sweden) ndio walioteuliwa. Nadine Angerer (Ujerumani), Marta (Brazil) na Abby Wambach (Marekani) ndio wagombea watatu wanaowania tuzo ya Mchezaji bora mwanamke.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman