Mgombea urais wa upinzani Congo Brazzaville afariki dunia
22 Machi 2021Mkuu wa kampeni ya Guy-Brice Parfait Kolelas, Christian Cyr Mayanda amesema kuwa mgombea huyo wa upinzani alifariki wakati alipokuwa kwenye ndege maalum ya kimatibabu kuelekea Ufaransa. Kifo cha Kolelas kimetokea siku hiyo hiyo ya uchaguzi baada ya kukutwa na ugonjwa wa Covid-19 siku tatu kabla ya uchaguzi.
Mayanda amesema kwamba kura zinaendelea kuhesabiwa na mgombea wao ameongoza kwenye baadhi ya vituo mjini Brazzaville na huko Pointe-Noire, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo na ngome ya mpinzani huyo.
''Mageuzi yatatokana na ukakamavu wenu''
Chama cha Kolelas kimeitisha mkutano wa hadhara leo mchana wa wafuasi wake ili kuwatangazia rasmi kifo chake. Jumamosi siku moja kabla ya uchaguzi, mgombea huyo wa upinzani alitangaza kupitia mkanda wa vidio, kuwa anapambana na kifo.
Lakini akawahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi, ili kuweko na mageuzi nchini Congo-Brazzaville. Aliwambia wafuasi wake kuwa mageuzi yatatokana na ukakamavu wao.
Guy-Brice Kolelas ndiye aliekuwa mpinzani mkuu kwenye uchaguzi wa hapo jana dhidi ya Rais Denis Ssassou Nguesso ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 36 sasa.
Kolelas mwenye umri wa miaka 60, alishika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa mwaka 2016. Wapinzani wengine, Jean-marie Mokoko na André Okombi wakitumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa tuhuma za kutishia usalama wa taifa.
Uchaguzi pasina waangalizi wa kimataifa
Uchaguzi wa jana Jumapili ulifanyika bila kuweko mawasiliano ya mtandao wa intaneti na ujumbe mfupi wa simu.
Hali hiyo imechochea kuongezeka kwa wasiwasi juu ya uwazi kwenye uchaguzi huo ambao hata hivyo unaonekana kumrejesha madarakani kiongozi wa muda mrefu Denis Sassou Nguesso. Kwa ujumla uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa siku chache zijazo.
Kanisa Katoliki lenye ushawishi na wafuasi wengi nchini humo, lilielezea wasiwasi wake pia kuhusu uwazi wa uchaguzi huo. Waangalizi wake wa uchaguzi walinyimwa vibali vya kufuatilia taratibu ya uchaguzi. Waangalizi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya pia hawakualikwa kufuatilia uchaguzi huo.
Kutokana na janga la Covid-19, Umoja wa Afrika, uliwatuma waangalizi wapatao ishirini pekee. Upinzani ulilalamikia taratibu ya uchaguzi na vilevile uchaguzi wa mapema kwa wanajeshi na maafisa wa idara za usalama.