IMF kuipatia Misri awamu ya kwanza ya mkopo uliopanuliwa
30 Machi 2024Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly amesema nchi hiyo itapokea awamu ya kwanza ya mkopo chini ya mkataba uliopanuliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF wiki ijayo. Ingawa hakutoa kiwango cha mkopo lakini IMF ilisema siku ya Ijumaa kwamba katika mpango wa kifedha uliopanuliwa wa dola bilioni 8 utawezesha shirika hilo kutoa mara moja kiasi cha dola milioni 820.
SomaUchumi wa dunia wayumba - IMF
Mkataba huo unapanua mpango wa ufadhili wa dola bilioni 3, wa miezi 46, uliotiwa saini Desemba mwaka 2022. Mkataba huo ulikuwa umesitishwa baada ya Misri kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuacha kudhibiti viwango vya ubadilishanaji wa sarafu yake, kuharakisha uuzaji wa mali za serikali na kutekeleza mageuzi mengine.
IMF ilikubali kutanua makubaliano hayo baada ya uchumi wa Misri kuathiriwa zaidi na mzozo wa vita vya Gaza, ambao ulipunguza kasi ya ukuaji katika sekta ya utalii na kusababisha mashambulizi kutoka Yemen, dhidi ya safari za meli katika bahari ya Shamu, na kupunguza kwa nusu mapato yatokanayo na mferereji wa Suez. Sekta ya utalii pamoja na usafiri wa meli ndiyo vyanzo vikuu vya fedha za kigeni kwa Misri.