Mapigano Mashariki mwa Kongo huenda yakashindwa kudhibitiwa
30 Juni 2022Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Bintou Keita ametoa tahadhari jana Jumatano kwamba mapigano yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo yanaweza kuongezeka na kushindwa kudhibitiwa.
Bintou Keita ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kongo na jana ameliambia baraza la usalama la Umoja huo kwamba ikiwa kundi la waasi la M23 litaendelea kufanya mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-FARDC na kikosi cha Umoja wa Mataifa,MONUSCO huenda wakajikuta wanakabiliwa na kitisho ambacho kitapindukia uwezo walionao hivi sasa.
Kongo nchi yenye utajiri mkubwa wa madini inapambana kuyadhibiti makundi chungunzima ya wanamgambo katika eneo la Mashariki,makundi ambayo mengi yametokana na vita viwili vya kikanda vilivyowahi kushuhudiwa robo karne iliyopita.
Uhasama
Mapigano makali yaliyozuka hivi karibuni huko mashariki yameufufua uhasama wa miongo kadhaa kati ya serikali ya mjini Kinshasa na Kigali,wakati Kongo ikiilaumu Rwanda kwa kuliibua upya na kuliunga mkono kundi la waasi la M23.Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Bintou Keita anasema harakati zinazoendelea za M23 na makundi mengine ya wanamgambo mashariki mwa nchi hiyo ni jambo linalotishia kurudisha nyuma hatua iliyopigwa katika suala la usalama na uthabiti nchini Jamhuri ya Kdemokrasia ya Kongo na katika kanda hiyo.
Rwanda mara kadhaa imekanusha kuwaunga mkono waasi wakati nchi zote mbili kila mmoja akimlaumu mwenzie kwa kufanya mashambulizi ya mpakani.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ameliomba baraza la usalama la Umoja huo kusaidia kurudisha amani mashariki mwa Kongo na kuiomba nchi hiyo na Rwanda kutafuta suluhisho. Lakini nchini Kongo zimekuwa zikisikika sauti za kuihimiza serikali mjini Kinshasa kufuta kabisa uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda. Martin Fayulu ni kiongozi wa Upinzani nchini Kongo.
"Tumeomba ubalozi wa Rwanda ufungwe,vijana wameomba hatua hiyo ichukuliwe,kila mmoja anaomba hilo,ikiwa nchi inakushambulia haiwezekani kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo''
Hata hivyo mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kongo Bintou Keita amesema mkutano wa kilele ujao wa Umoja wa Afrika utakaofanyika nchini Angola unapaswa kuwa fursa ya Kongo na Rwanda kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo.
Na wakati pia nchi nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwa zimekubaliana mwanzoni mwa mwezi huu kuunda kikosi maalum cha kikanda kitakachopelekwa mashariki mwa Kongo kusaidia kumaliza vita,Keita ametoa msisitizo kwamba kuna haja ya kuwepo ushirikiano na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa na ufafanuzi kuhusu majukumu na wajibu wa kila upande linapohusina na suala la kuwalinda raia wakati wa operesheni za baadae.
Kimsingi kwa mujibu wa mjumbe huyo kikosi cha kwanza kitakachopelekwa katika eneo hilo kinatarajiwa kabla ya mwishoni mwa mwezi Julai wakati kikosi kingine kimepangiwa kupelekwa mwezi Agosti.
Mwandishi:Saumu Mwasimba