Mkutano wa amani ya Syria kukamilika leo (31.01.2014)
31 Januari 2014Baada ya wiki nzima ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva, kati ya serikali ya Rais Bashar al-Assad na wajumbe wa upinzani, bado masuala muhimu hayajapatiwa ufumbuzi, likiwemo la kuundwa kwa serikali ya mpito na jinsi ya kuruhusu mashirika ya misaada kuingia katika mji uliogubikwa na mzozo wa Homs.
Jana Alhamisi (30.01.2014), mazungumzo hayo yalikwama baada ya pande hizo mbili kushindwa kukubaliana kuhusu nani anapaswa kulaumiwa kutokana na ghasia zinazoendelea nchini Syria.
Aidha, msuluhishi mkuu wa Umoja wa Mataifa na nchi za Kiarabu, Lakhdhar Brahimi amesema wajumbe walikubaliana kuwa suala la ugaidi ni tatizo kubwa ndani ya Syria, lakini hapakuwa na maafikiano jinsi ya kulitatua tatizo hilo.
Awamu nyingine kufanyika Februari, 10
Brahimi, amesema awamu nyingine ya mazungumzo hayo itaanza tena Februari 10 mwaka huu na kwamba ana matumaini katika mkutano huo pande zinazohasimiana zitafanikiwa kufikia makubaliano na kupata mfumo unaoeleweka.
Brahimi amesema mazungumzo hayo yalikuwa ni mwanzo wa mchakato muhimu wa awali ambapo pande hizo mbili zimekaa meza moja tangu kuzuka kwa mzozo huo Machi mwaka 2011 na kusababisha zaidi ya watu 130,000 kuuawa na kuwalazimisha mamilioni wengine kuyakimbia makaazi yao.
Wakati wa ziara yake mjini Berlin, kwa ajili ya kukutana na Kansela wa Ujerumani, Angela, Merkel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema kuwa mazungumzo hayo yamepiga hatua kadhaa, ingawa yanaonekana kuwa magumu.
Wanadiplomasia wanasema kuwa kipaumbele chao kikubwa ni kuona mchakato wa mazungumzo hayo unapiga hatua na kwamba wajumbe wake wanalegeza misimamo yao. Maafisa wa Marekani na wa Urusi ambao pia ni wafadhili wenza wa mkutano huo, wako mjini Geneva kutoa ushauri kwa upinzani na wajumbe wa serikali ya Syria.
Ajenda katika mkutano wa kwanza wa amani ya Syria uliopewa jina Geneva 1, uliofanyika mwaka 2012, zilihusisha masuala kadhaa kama vile kumaliza mapigano, kupeleka misaada na kufikiwa makubaliano ya kuunda serikali ya mpito.
Huku upinzani ukitaka kuanza kulizungumzia suala la serikali ya mpito, ambalo wanaamini litamuondoa madarakani Rais Assad, serikali ya Syria imesema hatua ya kwanza ni kulizungumzia suala la ugaidi.
Hata hivyo, katika kikao cha jana Alhamisi (30.01.2014), pande hizo mbili zilisimama na kukaa kimya kwa dakika moja ili kuwakumbuka maelfu ya watu waliouwawa katika vita vya nchi hiyo vilivyodumu kwa karibu miaka mitatu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu