Mkutano wa kujadili mabadiliko ya tabianchi mjini Berlin
18 Julai 2022Waziri Baerbock amesema mgogoro wa hali ya hewa hauna mipaka na ndio tatizo kubwa la kiusalama kwa watu wote katika dunia hii, na ndiyo maana majibu ya mgogoro huu wa hali ya hewa hayatakiwi pia kuwa na mipaka.
Mazungumzo ya Hali ya Hewa ya Petersberg ambayo yameandiliwa kwa pamoja na Ujerumani na Misri ni msingi wa kuandaa Mkutano wenye mafanikio wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa mwaka 2022 ambao kwa kawaida hujulikana kama COP27, ambao utafanyika mwezi Novemba katika mji wa pwani wa Misri wa Sharm el-Sheikh.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema sote tuko kwenye mashua moja na kuongeza kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine uliashiria kurudi nyuma kwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Amesema katika miezi ijayo, Ujerumani itatumia zaidi makaa ya mawe kwenye mitambo yake ya kuzalisha umeme lakini imeanzisha pia mikakati ya nishati mbadala.
"Ingawa haikuwa nia ya Putin, vita hivi vya kikatili na vya uchokozi ni kichocheo cha nishati mbadala. Sisi nchini Ujerumani tumeanzisha sheria kabambe ya nishati mbadala ambayo hatujawahi kuwa nayo na hapa kwenye Mazungumzo ya Hali ya Hewa ya Petersberg, tunashawishi kuimarisha maendeleo ya nishati mbadala duniani kote kwa ushirikiano na nchi nyengine."
Akizungumza katika mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ameelezea wasiwasi wake kutokana na mwamko wa kimataifa wa kurejelea vyanzo vya nishati chafuzi kwa mazingira hususan makaa ya mawe, unaotokana na upungufu wa gesi baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Wito wa Umoja wa Mataifa
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi badala ya kuwa na "mchezo wa kutupiana lawama". Guterres amesema itakuwa vigumu kuyafikia malengo ya kikomo cha ongezeko la joto cha 1.5 Celsius waliyoafikiana katika Makubaliano ya hali ya hewa ya mjini Paris mwaka 2015, katika kipindi hiki watu wakikabiliwa na mafuriko makubwa, ukame, dhoruba na mioto ya misitu.
Wanasayansi wanasema joto kali linaloshuhudiwa sehemu kubwa ya kaskazini mwa ulimwengu katika wiki za hivi karibuni inaweza kuwa hali mpya na ya kawaida katika majira ya kiangazi ikiwa ongezeko la joto duniani litaendelea.
Soma zaidi: COP26: Makubaliano yalegeza msimamo kuhusu makaa ya mawe
Kulingana na utafiti uliyotolewa leo na Wizara ya Uchumi wakati Mazungumzo ya Hali ya Hewa ya Petersburg yakiendelea mjini Berlin, Mabadiliko ya hali ya hewa yameigharimu Ujerumani wastani wa Euro bilioni 6.7 kwa mwaka tangu mwaka 2000. Gharama ya jumla tangu wakati huo imefikia bilioni 145.
(DPAE, APE)