Mkuu wa kikosi cha EAC nchini DRC ajiuzulu
28 Aprili 2023Taarifa iliyotufikia hivi punde inasema kuwa kujiuzulu kwa jenerali huyo kunakuja siku moja tu baada ya serikali ya Kongo kuitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya marekebisho muhimu kwenye kanuni zinazoongoza operesheni ya kikosi cha Umoja huo mashariki mwa Kongo ili kuepusha kile Kinshasa inachosema ni "hali ya kuchanganya."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Christophe Lutundula, aliwaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba nchi yake imeionya Jumuiya hiyo kwamba utendaji kazi wa kikosi chake unatia mashaka. Lutundula alikuwa akizungumza mara baada ya mkutano uliowaleta pamoja wajumbe kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na serikali ya Kongo kutathmini mchakato wa amani wa mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti zinasema Rais Félix Tshisekedi hakupendezewa na msimamo wa Jenerali Nyagah kukataa kuwaamuru wanajeshi wa kikosi chake kupambana na waasi wa M23, huku mwenyewe akisema ametishiwa mara kadhaa na "mamluki" kutokana na shinikizo la kisiasa.