Mrengo wa kulia watazamia mapinduzi kura ya rais Romania
24 Novemba 2024Waromania wanapiga kura Jumapili katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais katikati mwa mfumuko mkubwa wa bei ambao unaweza kumnufaisha kiongozi wa mrengo wa kulia, George Simion.
Kura hiyo inazindua wiki mbili za uchaguzi nchini Romania, ikiwemo uchaguzi wa bunge na duru ya pili ya uchaguzi wa rais Desemba 8.
Miongoni mwa wagombea 13 wa urais, Waziri Mkuu wa chama cha Social Democratic, Marcel Ciolacu, anaongoza kwa asilimia 25, akifuatiwa na kiongozi wa chama cha AUR, Simion, akiwa na asilimia 15-19.
"Ninaogopa sana tutamaliza na Simion katika duru ya pili," alisema mfanyakazi wa Tehama Oana Diaconu mwenye umri wa miaka 36, wakati akizungumza na AFP mjini Bucharest, akionesha wasiwasi kuhusu tabia isiyotarajiwa ya kiongozi huyo wa mrengo wa kulia na mashambulizi yake dhidi ya Umoja wa Ulaya.
Simion, mwenye umri wa miaka 38, anadai nafasi katika nchi maskini mwanachama wa NATO huku vyama vya mrengo wa kulia kote Ulaya vikishinda uchaguzi.
Kwa mujibu wa wataalamu, hatari ni kubwa katika kinyang'anyiro cha kumrithi Rais Klaus Iohannis, kiongozi wa mrengo wa kiliberali na mshirika mkubwa wa Ukraine, ambaye ameshikilia nafasi hiyo ambayo ni ya heshima zaidi tangu 2014.
Romania katika nafasi muhimu ya kimkakati kwa NATO
Romania, ambayo inapakana na Ukraine, imekuwa na umuhimu mkubwa tangu Moscow ilipovamia jirani yake mwaka 2022.
Nchi hiyo ya Bahari Nyeusi sasa ina nafasi ya "kimkakati muhimu" kwa NATO -- kwa kuwa inahifadhi zaidi ya wanajeshi 5,000 -- na ni njia ya usafirishaji wa nafaka za Ukraine, limesema shirika la utafiti la New Strategy Center katika utafiti wake.
"Demokrasia ya Romania iko hatarini kwa mara ya kwanza tangu anguko la ukomunisti mwaka 1989," alisema mchambuzi wa kisiasa Cristian Pirvulescu alipozungumza na AFP.
Soma pia:Rais wa Romania, Iohannis kuwania uongozi wa juu wa NATO
Baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani, "hali imekuwa ngumu zaidi", aliongeza.
Simion, anayejulikana kwa hotuba zake kali na shabiki wa Trump ambaye wakati mwingine huvaa kofia nyekundu kumuenzi kiongozi wake huyo - anatarajia kuimarishwa na ushindi wa Trump.
Simioni ambaye anapigania "Romania yenye uzalendo zaidi", anapinga kutuma msaada wa kijeshi kwa Ukraine na mara kwa mara hukosoa kile anachokiita "kiotoa cha rushwa na ufisadi" huko Brussels.
Romania hadi sasa imekuwa na "wasindikizaji na waoga kama viongozi," alisema hivi karibuni, na kuongeza kuwa watu "hawakubali tena kutendewa kama raia wa daraja la pili" katika nchi nyingine.
Simion afaidika na hasira za wapiga kura, Ciolacu aahidi utulivu
Simion ameshudia umaarufu wake ukiongezeka kwa kutumia hasira za wapiga kura juu ya mfumuko wa bei ulioweka rekodi huku akiahidi kutoa nyumba za bei nafuu kwa wote.
Katika juhudi za kupata uungwaji mkono kutoka Waromania wengi walioko nje ya nchi, amesafiri kote Ulaya.
Iwapo atafikia duru ya pili, mchambuzi Pirvulescu anatabiri "athari kubwa" ambayo huenda ikakipa msukumo chama chake cha AUR katika uchaguzi wa bunge wa Desemba.
Kwa ujumla, kampeni imekuwa na mizozo na mashambulizi ya kibinafsi, huku Simion akikabiliwa na tuhuma za kukutana na majasusi wa Urusi -- madai ambayo amekana.
Kwa upande mwingine, Ciolacu amekabiliwa na mzozo juu ya matumizi yake ya ndege za kibinafsi.
Soma pia: Romania na Bulgaria zajiunga kwa sehemu katika kanda ya Schengen
Pamoja na viwango vya umaarufu vya chini, anatarajia kuwashawishi wapiga kura kwa ahadi yake ya kuhakikisha "utulivu" nchini Romania.
Kama kiongozi wa Chama cha Social Democratic (PSD), Ciolacu anafurahia kuungwa mkono na chama kikubwa zaidi cha Romania, ambacho kimeunda siasa za nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu, na kwa sasa kinatawala kwa ushirikiano na Chama cha Kitaifa cha Kiliberali.
Anayeshika nafasi ya tatu ni mwandishi wa habari wa zamani Elena Lasconi, ambaye alikua meya wa mji mdogo wa Campulung na mkuu wa chama cha upinzani cha mrengo wa kulia, ambaye anaweza kutoa mshangao.
"Matarajio yetu ni kuwa kumalizia na Lasconi katika duru ya pili -- anaonekana kuwa mgombea mwaminifu zaidi," alisema mtaalamu wa Tehama Diaconu kabla ya kupanda kwenye tram huko Bucharest.