Mripuko wa kipindupindu Kenya
24 Mei 2023Takriban watu 70 wakiendelea kupokea matibabu katika majimbo ya Siaya na Homabay yaliyopo eneo la Nyanza Magharibi mwa Kenya huku maafisa wa afya wakichukua hatua katika baadhi ya sehemu kwenye eneo la Bonde la Ufa.
Matukio ya mikurupuko ya ugonjwa wa Kipindupindu yamekuwa yakishuhudiwa katika sehemu maeneo mbali mbali nchini Kenya kuanzia mapema mwaka huu 2023, baadhi ya maeneo yaliyoripoti na kudhibiti maradhi haya ni Kisumu na Kaskazini Mashariki mwa taifa.
Katika matukio ya hivi karibuni majimbo ya Homabay, Siaya na Kiambu yamegonga vichwa vya habari maafisa wa afya wakichukua hatua za dharura kudhibiti kusambaa kwa maradhi hayo yanayosabishwa na uchafu kupenya katika mikondo ya maji.
Kulingana na afisa msimamizi idara ya afya jimbo la Homabay, Dkt. Kevin Osuri tayari mtoto mmoja ameripotiwa kufariki huku watu 73 wakiendelea na matibabu, Ufuo wa Wadianga Ziwa Victoria eneo la Suba Kaskazini likiathirika zaidi na maambukizi.
"Tumechukua hatua za kuwafikia raia hadi maeneo ya nyumbani," amesema daktari Kevin.
Afisa msimamizi wa afya Jimbo la Uasin Gishu Joyce Muten ameelezea hatua walizochukua kuzuia makali ya ugonjwa huo eneo hilo ikiwa ni pamoja na migahawa 3 kufungwa Eldoret mjini, baada ya kubainika kuwa na mfumo mbovu wa kupitisha maji taka.
Sehemu nyingine iliyoathirika ni jimbo la Kiambu ambapo watu wanane walilazwa kutokana na ugonjwa huo siku 3 zilizopita.
Mnamo mwezi Aprili, watu 2 walifariki jimboni Kisumu wengine 7 wakilazwa kutokana na Kipindu pindu, sawia na wafungwa 47 wakipata maambukizi katika gereza la Thika.