Msumbiji yahimizwa kutumia nguvu kwa busara
11 Juni 2021Shirika hilo lenye makao yake nchini Ubelgiji, limeitaka Msumbiji kutumia nguvu kwa busara katika kukabiliana na kampeni kali inayoibuka katika eneo lake la kaskazini lenye utajiri mkubwa wa gesi. Katika ripoti yake, shirika hilo limesema kuwa mamlaka ya nchi hiyo inapaswa kukubali usaidizi wa kijeshi kutoka nje katika kukabiliana na uasi na kuwalinda raia waliopoteza makaazi.
Dino Mahtani, mwandishi wa ripoti hiyo, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kunapaswa kuwa na kiwango kinachokubalika cha kutoa shinikizo kwa kundi hilo la wanamgambo ili liweze kufikiria kujisalimisha na pia kuwapa njia ya kujitoa katika uasi. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa Msumbiji inapaswa kutatua masuala ya nchi hiyo ambayo yamesababisha makundi hayo kuleta ghasia ili kuweza kuzizuia. Kundi la itikadi kali yenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) linalojulikana nchini humo kamaAl-.Shabablimekuwa likilihangaisha eneo maskini la Cabo Delgado tangu mwaka 2017 kwa kufanya mashambulizi katika vijiji na miji.
Ghasia hiyo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,800 nusu ya idadi hiyo wakiwa raia. Mnamo mwezi Machi, wapiganaji walishambulia mji wa Palma na kuvilemea vikosi vya uslama na kusababisha kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa Total kukatiza shughuli zake katika mradi wa gesi ulioko karibu.
UNHCR yatoa takwimu
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), limesema kuwa watu wapatao 70,000 wameukimbia mji wa Palma tangu shambulio hilo kufanyika na kuongeza idadi ya waliopoteza makaazi kufikia takribani laki 8. Shirika hilo limesema kuwa maelfu ya watu wamekwama katika maeneo hatari huko Palma ambayo ni vigumu kufikiwa huku wengine wakijaribu kuvuka katika taifa jirani la Tanzania. Mashambulio hayo yaliosababisha vifo vya mamia ya watu, yanachukuliwa kuwa kitendo kibaya zaidi cha uasi wa makundi hayo ya itikadi kali katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Shirika la ICG limeihimiza serikali kutumia pesa za wafadhili kufadhili maendeleo ambayo huenda yakapunguza mvutano katika eneo hilo na kutoa mbinu mbadala za kujikimu kimaisha kwa watu maskini na wasiokuwa na ajira wanaovutiwa na makundi hayo. Mahatni amesema kuwa eneo la Cabo Delgado linalopakana na Tanzania na lililo umbali wa kilomita 1500 kutoka mji mkuu Maputo, limechochea uasi huo kutokana na masuala tete ya kiuchumi na kijamii.
Kilichochea uasi
Hali ya kukosa matumaini ilianza kuongezeka wakati jamii za eneo hilo zilipoanza kujihisi kutengwa kutoka kwa uvumbuzi wa gesi asilia na madini ya rubi. Vijana wakaanza kufanya uasi dhidi ya viongozi wa kidini katika eneo hilo lililo na idadi kubwa ya Waislamu. Mahtani amesema kuwa msaada utafungua fursa ya mazungumzo yanayohitajika kwa haraka na makundi hayo ya kijihadi na kufungua njia ya mazungumzo kuhusu uwezekano wa msamaha. Kufikia sasa, serikali ya Msumbiji imeangazia zaidi hatua za kijeshi.
Lakini rais wake Filipe Nyusi, anaonekana anachelea kuhusu kukubali msaada kutoka kwa majirani zake wa kikanda na mataifa ya magharibi. Shirika la ICG limemhimiza Nyusi kukubali msaada wa kipimo kutoka nje kusaidia na kutoa mafunzo kwa vikosi vya kijeshi nchini humo kuepukana na kuletwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi kutoka nje. Mahtani ameonya kuwa hali hiyo huenda ikaishia kuvutia wanamgambo wa kimataifa kujitokeza kupigana kuhusu muingilio wa kimataifa.