Muhammad Yunus kuongoza serikali ya mpito Bangladesh
7 Agosti 2024Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Muhammad Yunus amechaguliwa kuongoza serikali ya mpito ya Bangladesh. Hatua hiyo inafuatia kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Sheikh Hasina kujiuzulu na kukimbilia nje ya nchi katikati mwa maandamano ya kupinga utawala wake.
Akijulikana kama mkombozi wa maskini na mkosoaji mkubwa wa Hasina, Yunus atahudumu kama kiongozi wa serikali ya mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.Jeshi lachukua udhibiti wa Bangladesh
Uamuzi huo ulitangazwa baada ya mkutano uliofanyika jana jioni na kujumuisha viongozi wa maandamano ya wanafunzi, wakuu wa kijeshi, wawakilishi wa asasi za kiraia na viongozi wa wafanyabiashara.
Hadi sasa jeshi limechukua udhibiti, lakini haijulikani upi utakuwa ni wajibu wake katika serikali ya mpito baada ya rais Mohammed Shahabuddin kulivunja bunge na kupisha njia ya kuandaliwa uchaguzi mpya wa kumpata waziri mkuu.